KIPA wa Tabora United, John Noble amesema Yanga ilistahili kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, akitaja sababu ni ubora na ilikuwa na kikosi cha wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kuamua matokeo.
Noble amesema Yanga imekuwa imara kila idara kuanzia kipa, mabeki, viungo na washambuliaji, jambo analoona limeinufanikisha kuchukua ubingwa huo.
“Mfano kipa wa timu hiyo, Djigui Diarra ana ujuzi mkubwa na anapenda wengine wanapofanya vizuri aliwahi kuniambia ananifuatilia na anapenda aina ya udakaji wangu, ila niendelee kusonga mbele na kujifunza vitu vipya kila siku,” amesema kipa huyo.
“Ila pia na mimi napenda aina ya uchezaji wake ana vitu vingi vya kujifunza kutoka kwake, kwanza anajiamini ndio maana ana uwezo wa kumwambia mwingine anafanya vizuri.
“Yanga ilikuwa na uhakika wa kushinda kila mechi, hilo linatokana na wachezaji wa ndani, kila mmoja alikuwa anafanya kazi yake kwa usahihi, ndio maana unaona timu yao imefungwa mabao machache (13), inamiliki mabao mengi (60) inaongoza kwa pointi (71) na imeshinda michezo mingi (23).”
Noble alikuwa kati ya makipa waliokuwa wakihusishwa kutakiwa na Simba alipoulizwa endapo klabu hiyo itahitaji huduma yake? Amejibu: “Nipo tayari, Simba ni klabu kubwa, hakuna mchezaji anayeweza akakataa kuichezea.”
Siyo mara ya kwanza kwa Diarra, kupongeza wachezaji wanaofanya vizuri nje ya timu yake, nje na Noble kipa mwingine aliyewahi kumpongeza ni kipa wa Coastal Union, Ley Matampi.
Matampi amewahi kukiri kwamba, “Diarra aliniambia nafanya kazi nzuri, hivyo natakiwa kuendelea kupambana zaidi.
Kocha wa makipa wa zamani wa Simba, Idd Pazi aliwazungumzia Matampi na Noble kwamba wana uwezo mkubwa wa kuitumikia Simba.
“Kama Simba itawahitaji makipa endapo akiondoka Ayoub Lakred kama tunavyosikia tetesi, basi mmojawapo ya hao, wanafaa kuitumikia Simba.”