Dar es Salaam. Katika kuongeza ushiriki wa wanawake kwenye sekta ya uchimbaji madini, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (NEC) mkoa wa Simiyu, Gungu Silanga amekabidhi leseni kwa wachimbaji kwa kundi hilo ili lifanye shughuli hizo kwa ufanisi.
Amesema amefikia uamuzi huo, baada ya kundi hilo mkoani hapo kumuomba leseni, jambo aliloridhia huku akieleza katika kuchagiza na kuleta maendeleo kwa jamii na Taifa kwa ujumla ni sababu ya kufanya hivyo.
Silanga ameeleza hayo juzi Jumamosi Mei 18, 2024 mbele ya Waziri wa Madini Anthony Mavunde aliyehudhuria hafla hiyo iliyofanyika mkoani hapo na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya madini wakiwemo wachimbaji.
“Mimi ni Mnec wa Simiyu, waliponifuata nikawaambia sawa lakini nendeni mkaunde kikundi kitakachokuwa na wawakilishi wa wilaya zote tano za mkoa huu. Kina mama hawa ni wasikivu walifanya hivyo.
“Waziri (Mavunde), nilikuwa mbishi kuwakabidhi hapo awali kwa sababu ilikuwa haileti taswira ya mkoa wa Simiyu na mimi ni Mnec wa mkoa nzima,” amesema.
Silanga amejenga hoja hiyo kwa kile alichokifafanua baada ya kina mama hao kukamilishia taratibu hizo aliwasiliana na ofisa madini aliyempa fomu za kukamilisha suala hilo la kuwapatia leseni zilizokabidhiwa.
“Nipo makini, natekeleza ilani ya CCM, ndio maana leo nimesimama hapa kwa kujidai na kuwakabidhi leseni hizi ili kuendelea na uchimbaji wa madini. Nakuahidi nitaendelea kuwalea kina mama hawa,” amesema.
Mnec huyo ametumia nafasi hiyo kumweleza Mavunde kuwa Simiyu haijawahi kuchimbwa hivyo wameombwa kupelekewa mashine za kisasa zitakazotumika katika mchakato huo ili kuondokana na suala la kubahatisha.
Naye, Mavunde amemshukuru Silanga kwa moyo wake wa uelewa na kufuata maelekezo ya Serikali kwa hatua hiyo kuwapa heshima heshima kina mama wa mkoa wa Simiyu.
“Umepandikiza mbegu kubwa sana, ulichokifanya kwa kina mama hawa kina maana kubwa katika uchumi, umekuwa muungwana, mstaarabu na msikivu kwa kuwajali wanawake wa Simiyu.
“Leseni hii ninayowakabidhi kina mama haitakuwa na maana kama hautawasimamia ili kuona matokeo ya mwisho kwao, nataka kuona maisha ya kina mama wa Simiyu kupitia sekta ya madini hii ndio furaha kubwa kwa sababu makaratasi haya (leseni) ninayo mengi ya kugawa,” amesema Mavunde.
Mavunde amesema kama leseni za uchimbaji wa madini haziwezi kutafsiri au kubadilisha maisha ya Mtanzania ni sawa sawa na karatasi yoyote iliyopo mtaani, ndio maana alimsisitizia Mnec kuwa mlezi wao.
“Uchimbaji ni gharama kubwa,Serikali inaangalia mipango mizuri ya kusaidia na kuwezesha kina mama na vijana kufanya uchimbaji na wizara itakusaidia Mnec,” amesema Mavunde.