Kiongozi Mkuu Iran amteua mrithi wa Rais Ebrahim

Kiongozi wa ngazi ya juu nchini Iran, Ayatollah Ali Khamenei, amemteua makamu wa kwanza wa rais wa Iran, Mohammad Mokhber, kuwa rais kufuatia kifo cha Rais Ebrahim Raisi katika ajali ya helikopta. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).

Makamu huyo wa rais amechukua madaraka hayo ikiwa zimesalia siku 50 kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu nchini humo.

Kwa mujibu wa katiba ya Iran, makamu wa kwanza wa rais anastahili kuchukua wadhifa huo iwapo rais atafariki, kuondolewa madarakani, kujiuzulu au kuwa mgonjwa kwa kpindi cha zaidi ya miezi miwili.

Raisi, ambaye alifariki katika ajali hiyo ya helikopta jana Jumapili pamoja na waziri wake wa mambo ya kigeni, Hussein Amir-Abdollahian na maofisa wengine wa serikali, alikuwa anakaribia mwisho wa muhula wake wa kwanza wa kipindi cha miaka minne kama rais.

Uchaguzi wa nchi hiyo, unatarajiwa kufanyika katika kipindi cha siku 50 kumchagua rais mwengine kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo.

Jopo linalojumuisha spika wa bunge, rais wa mahakama na makamu wa rais wamepewa majukumu ya kupanga uchaguzi mkuu wa kitaifa.

Mokhber (68), aliteuliwa kuwa makamu wa rais Raisi alipochukua wadhifa huo Agosti mwaka wa 2021.

Makamu huyo wa rais alizaliwa katika mji wa Dezful, Kusini Magharibi mwa jimbo la Khuzestan, ambapo alihudumu katika nafasi tofauti za serikali.

Raia nchini Iran hupiga kura kumchagua rais mpya baada ya kila miaka minne tangu taifa hilo la Kiislamu kufanya uchaguzi wake wa kwanza mwaka wa 1980.

Kila rais amepewa nafasi ya kuongoza kwa kipindi cha mihula miwili.

Related Posts