Tanga/Lindi. Wakati Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ikitahadharisha kuhusu kimbunga Ialy kinachotarajiwa kusababisha upepo mkali nchini kesho Jumanne, Mei 21, 2024, wananchi wanaofanya shughuli zao kwenye ukanda wa pwani wa Bahari ya Hindi wameeleza namna walivyojipanga huku wengine wakiendelea na shughuli zao kama kawaida.
Juzi, TMA ilitabiri kimbunga hicho kilichopo umbali wa kilomita 680 kutoka pwani ya Tanzania, kuwa kitasababisha mvua kubwa na upepo mkali kesho Jumanne.
Kabla ya tishio hili la kimbunga Ialy, Mei 1, 2024, TMA ilitoa tahadhari ya kuwapo kwa kimbunga Hidaya ambacho baadaye kilikosa nguvu baada ya kuingia pwani ya Bahari ya Hindi na kusababisha madhara machache ikiwemo mvua kubwa ya upepo katika maeneo ya Mafia, Mtwara na Kilwa.
Kutokana na tahadhari iliyotolewa na TMA, leo Mei 20, 2024, Mwananchi limepiga kambi kwenye ukanda wa pwani wa Bahari ya Hindi na kuzungumza na wananchi wanaofanya shughuli zao kwenye maeneo hayo.
Mkoani Tanga, baadhi ya wavuvi waliokuwa wakivua usiku uliopita, wameeleza kwamba baharini kuna upepo mkali ambao umewafanya wasitekeleze majukumu yao kikamilifu, jambo ambalo linashabihiana na utabiri uliotolewa.
Nahodha wa meli, Abdallah Msema ambae aliingia baharini kuvua samaki usiku wa kumkia leo Mei 20 amesema ni kweli upepo upo,na mawimbi yapo hivyo kama mvuvi atatumia chombo kidogo kinaweza kupata madhara.
“Upepo na mawimbi yake upo kweli, kama mtu huelewi kuendesha chombo vizuri, kinaweza kukuletea madhara, hivyo wote ambao wanataka kuingia baharini ni lazima wahakikishe vifaa vyao vya usafiri ni vizima na vinaweza kuhimili mawimbi,” amesema Msema.
Kwa upande wake, mvuvi, Idd Salim Idd amesema hali ya upatikanaji samaki imekuwa ya tabu kutokana na uwepo wa upepo mkali na mawimbi yaliopo baharini ambayo wanahisi yanasababishwa na uwepo wa kimbunga Ialy katika bahari ya Hindi.
Akizungumzia kimbunga hicho, mwenyekiti wa mazingira katika mwalo wa Deep Sea, Hamis Said amesema baadhi ya wavuvi na manahodha wanasema hali ya bahari si shwari, hivyo wanatakiwa kuzingatia taarifa ya tahadhari kutoka TMA.
Mwenyekiti huyo amewataka wavuvi ambao wapo eneo hilo kuanza kuchukua tahadhari mapema kutokana na dalili hizo walizoziona ikiwa ni pamoja na upepo na mawimbi makubwa baharini.
“Zipo taarifa kutoka mamlaka ya hali ya hewa kuhusu uwepo wa kimbunga Ialy ambapo kesho Jumanne, Mei 21, kutakuwa na mvua kubwa na upepo mkali, hivyo tumetoa tahadhari kwa wavuvi wetu kuwa makini na kufuatilia kwa ukaribu kuhusu kimbunga hicho, ni muhimu kujihadhari na ikibidi wasitishe kuingia baharini,” amesema.
Nahodha mwingine, Hamad Hamisi amesema tangu kutokea kwa kimbunga Hidaya, bado hali haijawa sawa pwani ya bahari ya Hindi katika maeneo wanayokwenda kuvua lakini ndani ya siku mbili zilizopita, hali imebadilika zaidi.
Amesema kwa sasa ni msimu wa pepo za kusi lakini zimebadilika kwani hali kama hizo zilitakiwa kutokea kuanzia Juni, badala yake zimeanza mwanzoni kabisa mwa Mei, jambo ambalo sio kawaida na yote ni kutokana na vimbunga vinavyotokea.
Ofisa Uvuvi soko la Samaki Deep Sea, Neema John amesema wanaendelea kuwapa elimu wavuvi kuhusiana na tahadhali zinazotolewa na Mamlaka ya Hali Tanzania kuhusu uwepo wa vimbunga.
Amesema wanaendelea kutoa elimu lakini baadhi ya wavuvi wamekuwa wakikaidi, hivyo kuwataka wasidharau taarifa zote za tahadhali zinazotolewa na badala yake wafuatilie na kujihadhari na kimbunga hicho.
Kwingineko mkoani Lindi, Mwananchi limetembelea eneo la bahari na kukuta wavuvi wakiendelea na shughuli zao za kila siku, licha ya TMA kutoa tahadhari kuhusu kimbunga hicho kinachotarajiwa kesho.
Mvuvi katika pwani ya Ndoro, Salumu Yusuph amesema tangu juzi baada ya kusikia kuna kimbunga kingine kinakuja, baadhi ya wavuvi wameacha kwenda bahari hadi pale bahari itakapokaa sawa, lakini wenzao wengine wamekwenda bila kuchukua tahadhari zozote.
“Sisi wavuvi, kila mtu ana akili yake, mimi na baadhi ya wenzangu tumeamua kupumzika baada ya kusikia taarifa ya kuwepo kwa kimbunga kingine, lakini kuna wale wabishi, wao wameamua kwenda kwa madai kuwa njaa ndiyo imewasukuma kufanya hivyo.
“Hapa pwani yetu hatuna vifaa vya uokoaji, unaposema uende ukapata matatizo, nani atakayekuja kukuokoa, mwishowe unapoteza maisha kwa jambo ambalo ungeweza kujiokoa toka mwanzo,” amesema Yusuph.
Wanunuzi wa samaki wanasemaje
Mnunuzi wa samaki, Hamisi Jafari amesema baada ya kutangazwa kuwa na kimbunga Ialy, samaki wamekuwa hawapatikani kwa wingi kutokana na upepo mwingi baharini na imesababisha samaki aina ya jodari kupanda bei.
Amesema awali samaki hao walikuwa wananunua mmoja Sh120,000 kwa lakini tangu jana wananunua kwa Sh150,000.
“Baada ya kusikia kwenye vyombo vya habari kama kutakuwa na kimbunga kingine, baadhi ya wavuvi wameacha kwenda baharini, lakini haohao wanaoenda wanauza samaki kwa bei kubwa, kama jodari mwanzoni tulikuwa tunanunua Sh120,000 lakini tangu juzi tunanunua Sh150,000,” amesema Jafari.
Kwa upande wake, Shida Jumaa amesema tangu wametangaza kuwepo kwa kimbunga kingine, samaki hawapatikani na juzi alishindwa kabisa kununua samaki na akarudi nyumbani kutokana na bei kuwa kubwa.
“Mimi nauza sana samaki wa vipande aina ya jodari, lakini juzi nilishindwa kununua kutokana na kuwa bei juu, ikanibidi nirudi nyumbani, leo nimekuja tena, sijajua kama nitapata maana hadi saa hizi vyombo vilivyoenda havijarudi bado,” amesema Shida.
Wakati tahadhari zikiendelea kutolewa, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Lindi, Joseph Mwasabeja amesema wametoa taarifa kwa wavuvi kutokwenda bahari hadi pale hali itakapokuwa sawa.
“Nimetuma timu yangu kwenda kuwapa taarifa wavuvi wote wanaovua katika bahari ya Hindi, sitaki kumuona mvuvi anakwenda kuvua baharini hadi pale hali itakapokuwa shwari,” amesema Mwasabeja.
Imeandikwa na Rajabu Athumani na Bahati Mwatesa