Kutoka kilio hadi kicheko cha maji Uhambingeto

Iringa. Wakazi wa Kijiji cha Uhambingeto, Jimbo la Kilolo mkoani Iringa wamempokea Naibu Waziri wa Maji, Kundo Mathew kwa shangwe na nderemo baada ya kuanza kupata maji kijijini humo.

Mwaka 2023, wananchi hao walimpokea aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo kwa kuangua vilio wakilalamika kukwama kwa mradi wa maji.

Baadaye, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alikwenda kuwaomba radhi akiahidi maji yangetoka ndani ya muda mfupi.

Aweso aliuagiza Wakala wa Maji Vijijini (Ruwasa) Mkoa wa Iringa kusimamia mradi huo ambao ulikwama chini ya mkandarasi licha fedha kutolewa.

Mei 18, 2024 saa 2 usiku, Naibu Waziri wa Maji, alipokelewa kwa shangwe na wananchi hao wakishukuru kwa kupatiwa huduma ya maji.

Akizungumza kijijini hapo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Uhambingeto, Yohana Lyandala amesema maji ndiyo kero kubwa iliyokuwa ikiwatesa.

“Tulilia mwanzoni wakati maji hayatoki, ndoo moja ya maji ilikuwa inauzwa hadi Sh5,000 lakini, maji kwa sasa yanatoka. Hatuidai Serikali,” amesema Lyandala.

Baadhi ya wanawake wamesema hali ya ndoa zao ilikuwa taabani kutokana na kutumia muda mrefu kutafuta maji.

“Hata nguo zilikuwa hazitakati, unafuaje na maji ya chumvi? Maji ya kawaida ndoo ilikuwa bei kubwa sana na kupata maji pia ilikuwa changamoto,” amesema Atu Beni, mkazi wa Uhambungeto.

Kwa upande wake, diwani wa kata ya Uhambingeto, Tulinumtwa Mlangwa ambaye alikuwa miongoni mwa wananchi walioangua kilio wakati wakiomba maji, amesema hana neno baada ya kupata maji.

“Tangu mchana tunakusubiri kushukuru, hata ilipofika saa 1 usiku tulibaki hapahapa uje kiongozi wetu, tunashukuru kwa ujio wa maji,” amesema Mlangwa.

Mbunge wa Kilolo (CCM), Justine Nyamoga amesema Kihorogota ni kati ya vijiji vilivyokuwa na changamoto kubwa ya maji.

“Nimehangaika kuhakikisha Uhambingeto wanapata maji na hiki lilikuwa kilio chao kikubwa,” amesema Nyamoga.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew amesema lengo la ziara yake ilikuwa ni kuona kama maji yanatoka.

“Maji yanatoka, hongereni sana kwa hili, Serikali yenu ni sikivu na pamoja na kuwa ni usiku, ratiba ilinibana lakini nimekuja. Tunzeni maji haya, tunzeni miundombinu hii,” amesema Mathew.

Kundo amesema zaidi ya miradi saba ya maji inatejelezwa kwenye jimbo hilo ili kufikia malengo ya wananchi wote kupata maji.

Related Posts