LIGI Kuu ya Zanzibar (ZPL) inazidi kuyoyoma, huku ikishuhudiwa idadi ya hat trick zikiongezeka baada ya jana Jumapili kupigwa nyingine mbili na kufanya idadi sasa ifikie sita wakati timu za Mlandege na Zimamoto zikipata ushindi mnono mbele ya vibonde Maendeleo na Jamhuri za Pemba.
Mohamed Ali Mohamed wa Mlandege na Mgaza Seleman Ramadhan wa Zimamoto ndio walioongeza idadi ya ht trick katika Ligi ya Zenji.
Wengine waliofunga hat trick hadi sasa ni, Mudrik Miraji Mawia wa JKU, Ibrahim Hamad ‘Hilika’ wa Zimamoto, Ibrahi,m Is-haka wa KMKM na Suleiman Mwalim Abdalla wa KVZ ambaye Alhamisi iliyopita alifunga mabao manne na kuweka rekodi ya kuwa nyota pekee aliyefunga idadi hiyo katika mechi moja.
Mlandege ikiwa kwenye Uwanja wa Amaan Kwa Wazee, Unguja ilipata ushindi wa mabao 5-2 dhidi ya waburuza mkia, Maendeleo, huku Zimamoto ikiifumua Jamhuri kwa mabao 3-0 katika pambano jingine lililochezwa Uwanja wa Mao A, mjini Unguja.
Ushindi iliyopata Zimamoto umeifanya ichupe kutoka nafasi ya nne hadi ya pili kwa kufikisha pointi 50 kupitia michezo 24, ikiwa nyuma ya vinara JKU yenye alama 53, wakati Mlandege ikichupa kutoka nafasi ya 11 hadi ya nane kwa kukusanya pointi 30, ilihali Maendeleo na Jamhuri zikizidi kujiweka pabaya katika janga la kushuka daraja, kwani zimeendelea kusalia eneo la mkiani.
Maendeleo ndio inayoburuza mkia ikiwa na pointi 15 tu, huku Jamhuri ikiwa nafasi ya pili toka chini katika ligi hiyo yenye timu 16, ikivuna pointi 18 kila moja ikicheza jumla ya mechi 25 hadi sasa.
Katika mchezo uliopigwa Amaan, mshambuliaji Moh’d Ali Moh’d alifunga hat trick yake kwa mabao ya dakika za sita, 35 na 46, huku Mussa Salum na Fahad Hassan kila mmoja alifunga bao moja dakika ya nne na 87 na kuipa Mladende ushindi humo mnono wa mabao 5-2.
Mabao ya kufutia machozi ya Maendeleo yaliwekwa kimiani na David Goodluck Sovela katika dakika ya 48 na 75′ na kumfanya afikishe jumla ya mabao saba kwa msimu huu wa ligi hiyo ya Zanzibar, akilingana na Ramadhan Amri Mponda (Malindi), Abdulhamid Juma Abdi (Kundemba) na Mudrik Abdi Shehe (JKU).
Kinara wa mabao kwa sasa katika ligi hiyo ni Suleiman Mwalim Abdallah wa KZV mwenye mabao 19, kifuatiwa na Ibrahim Hamad ‘Hilika’ wa Zimamoto mwenye 14, huku Ibrahm Is-haka wa KMKM na Yazidu Idd Mangosogo wa New City wakiwa na mwbao 10 kila mmoja katika nafasi ya tatu.
Nyota hao wanafuatiwa kwa karibu na Arqam Ahmed Zubeir (Kipanga) na Omari Thani Abdalla (Malindi) ambao kila mmoja amefunga manane.
Katika mechi iliyopigwa Uwanja ww Mao A, Mgaza aliizamisha Jamhuri kwa mabao ya dakika 39, 46 na 48.
Mabao hayo yamemfanya mchezaji huyo kufikisha manne msimu huu, lakini akiiweka pabaya Jamhuri ambayo iwapo haitakomaa mechi tano ilizonazo mkononi itashuka daraja kama ilivyo kwa Maendeleo.
Timu nyingine zilizopo kwenye mstari mwekundu na kuhitajika kufanya kazi ya ziada kwa mechi ilizonazo mkononi kabla ya msimu kufungwa rasmi katikati ya Juni ni, Ngome yenye pointi 20 na Kundemba yenye alama 23.
Kwa mujibu wa kanuni ya Ligi Kuu Zanzibar, timu nne za mwisho katika msimamo zinashuka moja wa moja kwenda Ligi Daraja la Kwanza Taifa.
Ngome ni kati ya timu nne zilizopanda daraja msimu huu sambamba na New City, Chipukizi na Maendeleo, zilizochukua nafasi ya Black Sailors, Polisi, Taifa Jang’ombe na Dulla Boys zilizoshuka msimu uliopita kwa kushika nafasi nne za chini za msimamo wa ligi hiyo ulioshuhudia mabingwa wa kihistoria, KMKM ikibeba taji la tatu mfululizo