Mafuriko Manyara yasababisha 600 kukosa makazi

Babati. Watu 600 wa kijiji cha Manyara, wilayani Babati mkoani Manyara, wamekosa mahali pakuishi baada ya makazi yao kukumbwa na mafuriko.

Pamoja na kukosa makazi kwa kukumbwa na mafuriko watu hao pia mashamba yao yamesombwa na maji na kuharibu mazao yao.

Mwenyekiti wa kijiji cha Manyara, Juma Jorojik ambacho kimepakana na ziwa Manyara, akizungumza Mei 20 amesema wananchi wa eneo hilo wana hali tete kutokana na tukio hilo.

Jorojik amesema watu 600 wa kijiji hicho hawana mahali pakuishi baada ya nyumba zao kufunikwa na maji yaliyotokana na mafuriko hayo.

Amesema mashamba yao yakiwa na mazao ikiwemo mahindi, maharage, ufuta na mengine yamefunikwa na maji yaliyotokana na mafuriko hayo.

Amesema chanzo cha mafuriko hayo ni mvua zinazonyesha kupeleka maji ziwa Manyara na kuingiza kwenye kijiji chao hivyo kuzua sintofahamu na taharuki kwa wakazi wa eneo hilo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na mbunge wa Babati vijijini, Daniel Sillo ametoa magunia 10 ya mahindi ya chakula kwa waathirika wa mafuriko waliopo katika kijiji hicho.

Naibu Waziri Sillo ametembelea, kutoa pole kwa wapiga kura wake na kukagua uharibifu wa mali uliotokana na vyanzo mbalimbali vya ziwa Manyara kuzidiwa na mvua zinazoendelea kunyesha.

Hata hivyo, amewataka wakazi hao kupokea kiasi cha chakula kilichopatikana huku serikali ikiendelea kufanya jitihada nyingine za kutoa msaada zaidi.

“Ndugu zangu nipende kutoa pole kwa waathirika wa mafuriko kwani ni muda sasa wa kutumia chakula kilichokabidhiwa huku Serikali ikiendelea kufanya jitihada mbalimbali ili mpate nafuu,” amesema Sillo.

Ametoa onyo kwa tabia inayofanywa na baadhi ya makundi ya watu wasio na nia njema kwa kufanya udokozi kwani vyombo vya ulinzi na usalama vipo kazini.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Babati, Anna Mbogo amewaagiza wataalamu kuendelea kufanya tathmini ya maafa hayo

Mbogo amemtaka mganga mkuu wa halmashauri hiyo kuhakikisha wanachukua tahadhari kwa wananchi hao kuepuka magonjwa ya milipuko.

Hata hivyo, baadhi ya wakazi wa kijiji hicho wamemshukuru Sillo na wameipongeza Serikali kwa kuwa bega kwa bega katika kipindi kigumu.

Mmoja kati ya wakazi hao, Julius Salawe ameoimba Serikali kuendelea kupeleka msaada zaidi hasa wa vyakula kutokana na mazao yao kusombwa na maji.

(Imeandikwa na Joseph Lyimo)

Related Posts