Maswali manne ishu ya Phiri kutua Yanga

WAKATI Yanga ikisubiri kujua hatIma ya sakata la kimkataba la mshambuliaji wa Azam FC, Prince Dube Inayempigia hesabu za kumchukua mwisho wa msimu huu, mabosi wa Jangwani wamerudi kwa mshambuliaji, Moses Phiri kama mbadala wa Mzimbabwe huyo.

Yanga inamtaka Dube ambaye anaendelea kupambana na klabu yake akitaka kuachana nayo, lakini mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara wamejiweka tayari kumalizana naye baada ya hatima ya sakata hilo.

Hata hivyo, wakati Yanga ikisubiri hatima ya Dube inadaiwa kuanza mazungumzo na Phiri ikijiweka tayari kumchukua endapo tu kesi hiyo inayosubiri hatima ya uamuzi mbele wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya (TFF) ambayo ilisema kuwa ni suala la muda tu hukumu hiyo itatolewa.

Taarifa za ndani kutoka kwa mabosi wa Yanga ni kwamba, Phiri ambaye waliwahi kukaribia kumsainisha kabla ya kutua Simba miaka miwili iliyopita wanaamini kuwa ndiye mtu ambaye pia anaweza kuwasaidia kuongeza nguvu kwenye kikosi chao.

Hata hivyo, kuna maswali mengi ambayo ya kujiuliza kuhusu usajili wa nyota huyo kwa Yanga ya sasa.

Kwa mwenendo wa kikosi cha Yanga kwa sasa, wachezaji watatu wanaweza kuondolewa Skudu Makudubela, Kennedy Musonda na Joyce Lomarisa, ambapo kwa uhalisia Phiri anaweza kuingia kwenye nafasi ya wageni hao wawili wa juu.

Kiuhalisia ili Yanga iwe na uhakika wa kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa msimu ujao, itahitaji mshambuliaji aliye tayari kusaidiana na Joseph Guede, hivyo kama itamsajili Phiri itakuwa na nafasi moja tu kwenye eneo la ushambuliaji ambalo limekuwa likiisumbua kwa miaka ya hivi karibuni.

Kwa kiwango alichokuwa nacho Simba, Phiri akiingia badala ya Skudu anaweza kuwa na muda mfupi wa kucheza hadi atakapoanza kuzoeana kama kocha ataamua kumpa muda, lakini itategemea Yanga itamsajili mshambuliaji gani mwingine na uwezo wa huyo mgeni ambaye anaweza kuziba matumaini ya Mzambia huyo.

Siku za hivi karibuni Yanga imewasajili wachezaji wawili ambao waliwahi kucheza Simba, Jonas Mkude na Okrah ambao wote kwa pamoja wameshindwa kufanya vizuri kwenye kikosi hicho wakiwa hawana nafasi kwenye kikosi cha kwanza, hali hiyo inaweza kuwatisha Yanga kuhusu Phiri kuwa anaweza pia kukosa nafasi kwenye timu hiyo.

Kiuhalisia pamoja na mambo mengine mengi, Phiri aliondoka Simba baada ya kukosa nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza, ni kweli ambapo anaweza kucheza Yanga ambayo inaonekana kuwa na wachezaji wengi mahiri zaidi kuliko waliopo kikosi cha Simba? tusubiri tuone.

Mwanaspoti lilimtafuta Mzambia huyo kutaka kufahamu iwapo Yanga imebisha hodi mlangoni kwake na yeye akaweka wazi kuwa,” siwezi kuzungumza chochote kwa sasa kuhusu msimu ujao, tusubiri msimu huu umalizike kwanza ambapo nitakuwa nimeshamaliza mkataba (na Simba).”

Related Posts