Mtibwa Sugar mambo bado magumu

Timu ya Mtibwa Sugar leo imetoka ssuluhu na Namungo katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa kwenye uwanja wa Manungu Complex, Turiani, Morogoro jambo linalozidisha presha kuhakilisha inasalia kwenye ligi  msimu ujao baada ya kuwa kwenye nafasi ya mwisho katika msimamo.

Mtibwa Sugar baada ya mchezo huo uliochezwa kuanzia saa 8:00 mchana imefikisha alama 21 ambapo imebakiwa na michezo miwili na endapo itashinda yote itaishia kuwa na alama 27 na ili ibaki Ligi Kuu au kucheza mtoano (play off) itapaswa kuziombea matokeo mabaya Geita Gold na Tabora United kwenye michezo iliyosalia.

Timu hiyo ilipanda Ligi Kuu 1995 ambapo msimu wa 1999-2000 ilitwaa ubingwa wa ligi na tangu wakati huo haikuwahi kushuka daraja ambapo ni miaka 29.

Mtibwa Sugar ndiyo timu pekee nchini iliyofanikiwa kukuza na kulea vipaji vya wachezaji wengi ambapo miongoni mwao wanaofanya vizuri kwenye ligi ni pamoja na Dickson Job na Kibwana Shomari  wa Yanga pamoja na Mzamiru Yassin.

Endapo itashuka daraja msimu huu itaacha simanzi kwa vijana wenye vipaji vya soka mkoani Morogoro ambao waliifanya kuwa sehemu ya kutokea kimaisha kwani wale walioonekana kufanya vizuri waliitumia timu hiyo kama daraja la kufikia mafanikio yao.

Baada ya mchezo wa leo, Kocha wa timu hiyo, Zuberi Katwila amesema timu hiyo licha ya kupata sare ilipoteza nafasi nyingi za kufunga.

Related Posts