Mwili wa askofu anayedaiwa kujinyonga wawasili nyumbani kwa mazishi

Dodoma. Mwili wa aliyekuwa Askofu Mkuu wa Makanisa ya Methodist Tanzania (TMC) Joseph Bundala umewasili nyumbani kwake Ihumwa jijini Dodoma kwa ajili ya ibada ya maziko ambayo yatafanyika kwenye uwanja wa kanisa hilo leo Jumatatu, Mei 20, 2024.

Mwili wa askofu huyo umewasili nyumbani kwake saa sita mchana na kupokelewa na waombolezaji. Nyuso za majonzi zimetawala nyumbani hapo hususan jeneza lenye mwili wa kiongozi huyo wa kiroho ukiwasili.

Baada ya mwili huo kuingizwa ndani, tangazo limetolewa kwa viongozi wote wa dini wa makanisa ya Methodist pamoja na waliokuwa wafanyakazi wenzake na marehemu kuingia ndani ulipo mwili.

Awali, waombolezaji ambao pia ni washirika wa kanisa hilo wamesema msiba huo umewashtua sana kwani umekuja ghafla bila matarajio.

Kesia Sanze ambaye ni mshirika wa kanisa la Methodist Ipagala lilipotokea tukio la askofu huyo kudaiwa kujinyonga, amesema habari hizo ziliwashtua kwani hawakutegemea askofu huyo kujinyonga kutokana na alivyokuwa mcha Mungu.

Amesema tukio hilo limewahuzunisha na kuwafadhaisha kwani walikuwa wanamtegemea katika mambo mengi ya kanisa kwani ndiye aliyekuwa kiongozi mkuu hivyo kifo chake kimeacha simanzi kubwa.

Naye Peter George ambaye anatoka kanisa la Mapinduzi amesema walipokea taarifa za kifo cha askofu huyo kwa mshtuko mkubwa kwani tukio hilo hawakulitegemea.

“Lakini sote tunajua tutakufa na hapa duniani siyo makazi yetu ya kudumu kikubwa tu tujiulize tutaondokaje? maana kila mtu ana njia zake za kuondoka duniani hivyo tumwombe Mungu atupe mwisho mwema,” amesema George.

Akizungumza kuhusu ratiba ya mazishi, Katibu Mkuu wa kanisa hilo, Askofu Allen Siso amesema ratiba ya ibada inaenda vizuri kama ilivyopangwa ambapo muda huu waombolezaji wanapata chakula cha mchana kabla ya ibada kuanza.

Amesema ibada hiyo itafanyika hapo nyumbani na maziko yatafanyikia kanisani ambapo kaburi limeandaliwa huko.

Askofu Bundala anadaiwa kukutwa amejinyonga ndani ya choo kwenye ofisi yake iliyopo katika kanisa hilo eneo la Meriwa jijini Dodoma, Mei 16, 2024.

Tukio hilo linadaiwa kutokea saa 1 jioni na Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma likidai kiongozi huyo wa kiroho aliacha ujumbe ukieleza sababu za kujinyonga ni madeni aliyeokuwa nayo pamoja na mgogoro wa shule binafsi aliyoiuza.

Related Posts