Rais wa Iran, Ebrahim Raisi, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo na maofisa wengine wa serikali wamepatikana wakiwa wamefariki katika eneo la ajali ya helikopta baada ya msako wa saa kadhaa katika eneo lenye ukungu la milima kaskazini magharibi mwa nchi hiyo. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa …(endelea).
Vyombo vya habari vya serikali havikutoa sababu za haraka za ajali hiyo iliyokatisha uhai wa kiongozi huyo aliyekuwa na umri wa miaka 63.
Watu wote tisa waliokuwa kwenye helikopta hiyo walifariki wakati ilipoanguka katika jimbo la kaskazini-magharibi mwa Azerbaijan la Iran.
Naibu Rais wa Iran anayehusika na masuala ya Utendaji, Mohsen Mansouri pia amethibitisha kifo cha rais wa Iran.
Tukio hilo linakuja wakati Iran chini ya Raisi na Kiongozi Mkuu, Ali Khamenei ilianzisha shambulio ambalo halijawahi kushuhudiwa dhidi ya Israel mwezi uliopita na kurutubisha madini ya uranium karibu zaidi na viwango vya kiwango cha silaha.
Raisi na waziri wa nambo ya Nje, Amir Abdollahian walikuwa wakisafiri kurudi kutoka mkutano na Rais wa Azerbaijan, Ilham Aliyev. Helikopta hiyo ilitoweka kwenye rada jana Jumapili mchana.
Helikopta hiyo iliyombeba Raisi, ilianguka katika eneo la mbali kaskazini mwa Iran Jumapili jioni kutokana na hali mbaya ya hewa.
Hali mbaya ya hewa katika eneo hilo inatajwa pia kutatiza shughuli za utafutaji huku rais akiwa ametoweka kwa zaidi ya saa 12 kufikia mapema Jumatatu.
Nchi kadhaa zikiwemo Urusi na Uturuki zimetoa msaada katika operesheni ya uokoaji, huku ndege isiyo na rubani ya Uturuki pia ikiruka katika anga ya Iran kusaidia shughuli ya utafutaji.
Kiongozi wa juu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei amewatoa wito Wairan kumwombea Raisi.
Raisi aliapishwa kama rais mpya wa Iran mnamo Agosti 2021.
Alishinda uchaguzi wa urais mwezi Juni na chini ya asilimia 62 ya kura kama mgombea mkuu wa vyama vya siasa kali na anayependwa zaidi.
Alizaliwa mwaka wa 1960 huko Mashhad, kaskazini-mashariki mwa Iran.
Raisi alikuwa na ushawishi mkubwa ndani ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kudumisha uhusiano wa karibu na Khamenei.
Kwa mujibu wa katiba, Raisi ni kiongozi namba mbili nchini Iran, akimfuata Khamenei aliye mkuu wa nchi na pia ndiye mwenye uamuzi wa mwisho katika masuala yote ya kimkakati.