Serikali yawaondoa hofu Watanzania kuhusu soko la Kariakoo

Dodoma. Serikali imewaondoa hofu Watanzania kuwa Soko la Afrika Mashariki lilopo katika Jengo la China Plaza, Ubungo jijini, Dar es Salaam halitaua soko la Kariakoo.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu Mei 20, 2023 na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji wakati wa semina ya wabunge katika ukumbi wa Pius Msekwa.

Semina hiyo ilihusisha taasisi mbili zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Bishara ambazo ni Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela).

Amesema soko la Afrika Mashariki linalojengwa hapo Ubungo linazua hofu kwa wafanyabiashara wa Kariakoo na kwamba wamefanya vikao nao kwa zaidi ya mara tatu kujadiliana kuhusiana na jambo hilo.

“Sisi kama timu ya Serikali ipo kazini inafanya kazi yake, mheshimiwa mwenyekiti pale Ubongo Plaza yanajengwa maduka 2002, wakati Kariakoo kuna maduka 40,000.

Kama Serikali tunajaribu kuangalia hii hofu inatoka wapi, maduka 2002 yakaua maduka 40,000. Mheshimiwa mwenyekiti tunalifanyia kazi jambo hili,” amesema.

Amesema wizara yake inashirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ambao ndio wenye Manispaa ya Ubungo kuona mkataba walioingia, umeingiwaje na wanakwenda nao vipi.

Amesema lakini wanashirikiana pia na Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) kwa sababu wao ndio wanaotoa vibali vya ufanyaji kazi nchini kwa wageni.

Amesema lengo ni kujua Raia wa China wanaosemwa wanauza maua nchini, vibali vyao vinaonyesha wamekuja kufanya nini nchini.

“Je, alichosajili ndicho kifanya kwa hiyo timu ya Serikali mwenyekiti iko kazini na tunaelekea pazuri lakini pia tukikamilisha tutaileta bungeni,”amesema.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji , akizunguza na wabunge katika  semina iliyofaanyika  ukumbi wa Pius Msekwa.

Dk Kijaji amesema zipo taarifa kuwa asilimia 98 ya watu waliomba kufanya biashara kwenye maduka hayo ni Watanzania.

“Asilimia 98 ya wananchi waliochukua vibanda 2002 ni Watanzania sasa hiii inaendelea kutupa picha kwamba asilimia 98 ya waliochukua vibanda ni Watanzania, Wachina wanakujaje kuua soko letu,”amesema.

Amesema wanaendelea kulifanyia kazi kwa umakini mkubwa na itakapofikia Julai 2024 wakati ambapo maduka hayo yatafunguliwa itajulikana ukweli kuhusu jambo.

Awali, akichangia Mbunge wa Viti maalum Mwanaisha Ulenge aliuliza kuhusiana na jengo hilo linasemekana jengo hilo badala ya Watanzania Kwenda China watapata mahitaji katika jengo hilo.

“Tutakuwa tunachukulia pale (bidhaa) kama point of colletion, hofu iliyoko mtaani ni kwamba tunakwenda kuuwa soko la Kariakoo. Tunaomba kupata uelewa kwa niaba ya ndugu zetu waliopo Kariakoo,” amesema.

Akijibu hoja za wabunge, Mkurugenzi wa Idara ya Leseni wa Brela, Andrew Mkapa amesema kuna haja ya kutoa elimu kwa Watanzania ili wajue haki zao wakati wanaingia ubia na wawekezaji wa nje ya nchi wakati wa kusajili kampuni.

Amesema inakuwa ni vigumu kujua kama Mtanzania atadhulumiwa pia wanapofika kusajili kampuni na wageni hao.

Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk Athuman Ngenya amesema shirika hilo litaendelea kuboresha miundombinu na kuweka mazingira rafiki ya utoaji wa huduma kwa wakati ili kuchochea ufanyaji wa biashara na kuinua uchumi wa viwanda.

“Lengo ni kuchagiza uanzishwaji wa bidhaa salama na ubora hapa nchini kama njia mojawapo yakuchangia pato la Taifa,”amesema.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Brela,  Godfrey Nyaisa amesema katika kipindi cha miaka saba  kupitia mfumo wa usajili kieletroniki (ORS), kuna ongezeko la kampuni zilizosajiliwa kutoka 119,000 hadi kufikia 205,000, Mei 2024.

Naye Kaimu Mwenyekiti wa Bunge wa Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Dk Medard  Kalemani ameipongeza Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuzifanyia mageuzi makuubwa taasisi za TBS na Brela ambazo zilikuwa na changamoto kubwa ya kiutendaji.

Related Posts