SMZ kupima kupima utendaji kazi watumishi kidijitali

Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), itaanza kutumia Mfumo wa Kielektroniki wa Upimaji Utendaji Kazi (PA) ili kuongeza ufanisi katika taasisi za umma.

Kwa sasa Serikali inatumia fomu ya upimaji utendaji kazi (PAF) kuwapima watumishi wa taasisi za umma, ambapo utekelezaji wake ulianza tangu Novemba 2019 hadi sasa unaendelea.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba Sheria Utumishi na Utawala bora, Haroun Suleiman leo Jumatatu Mei 20, 2024 wakati wa mkutano wa 15 wa Baraza la Wawakilishi

Waziri alikuwa akijibu swali la mwakilishi wa Mtambwe, Dk Mohammed Ali Suleiman aliyetaka kujua mifumo gani ya tathmini ya utendaji kazi inayotumika kwa watumishi wa taasisi za umma hapa Zanzibar.

Dk Mohammed amesema pamoja na mfumo huu kuonekana kufanya kazi vyema katika mataifa mengi na kuongeza ufanisi, bado utekelezaji wa mfumo huu katika taasisi za umma hapa Zanzibar unasuasua.

Waziri Haroun amesema Serikali inatumia fomu ya upimaji utendaji kazi (PAF) kuwapima watumishi wa Taasisi za Umma hapa Zanzibar, ambapo utekelezaji wake ulianza tangu Novemba 2019 hadi sasa unaendelea.

“Ni kweli sasa ni muda mwafaka wa kuja na Mfumo wa Kielektroniki wa Upimaji Utendaji Kazi (Performance Appraisal) ili kuongeza ufanisi katika taasisi zetu,” amesema Waziri Haroun.

Hata hivyo, amesema wizara inaimarisha fomu hiyo kwa kuitoa katika mfumo wa manuali na kuwa ya kijiditali ili iunganishwe na ‘biometric’ za mahudhurio na kutoa matokeo halisi tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo alama hutolewa na kiongozi husika kwa namna anavyohisi yeye zaidi.

Related Posts