Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetabiri kimbunga “Ialy” kinapungua nguvu yake huku kikielekea kaskazini, mbali na pwani ya Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo jioni Jumatatu, Mei 20, 2024 na TMA kuonesha mwenendo wake imesema kimbunga hicho kinatarajiwa kuisha nguvu yake kabisa usiku wa kuamkia keshokutwa Jumatano, Mei 22, 2024.
“Kutokana na umbali kilipo kutoka nchini, vipindi vya upepo mkali vimeanza kujitokeza katika maeneo ya ukanda wa pwani kama ilivyotabiriwa.
‘’Kwa mfano, vituo vya hali ya hewa vilivyopo Unguja, Pemba na Mtwara vimeweza kuripoti upepo unaofika kilomita 50 kwa saa katika siku ya leo,” imesema TMA.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa kwa umma, matarajio yao vipindi vya upepo mkali unaozidi kilomita 40 kwa saa na mawimbi makubwa yanayozidi mita mbili vitaendelea kujitokeza katika maeneo ya ukanda wa pwani ya nchi.
“Na katika Bahari ya Hindi kati ya leo Mei 20, 2024 na usiku wa kuamkia Jumatano Mei 22,2024 kabla kimbunga “IALY” hakijaisha nguvu yake kabisa,” imeeleza TMA na kuongeza:
“Vipindi vya mvua vinaweza kujitokeza katika maeneo ya ukanda wa pwani (mikoa ya Tanga, Pwani (ikijumuisha Mafia), Dar es Salaam, Lindi na Mtwara pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba) kati ya kesho na kesho kutwa.”
Mamlaka hiyo imewashauri watumiaji wa bahari na wananchi wa maeneo ya ukanda wa pwani kuchukua tahadhari na kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka hiyo kwa kuzingatia miongozo ya wataalam wa kisekta.
TMA inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga hicho na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila inapobidi.