Vijana waaswa kushauri panapostahili sio kufanya uchawa

Dodoma. Changamoto za kiuchumi kwa vijana zimetajwa kuwa ni kikwazo kwa vijana wengi kushiriki kwenye chaguzi mbalimbali, huku wakitakiwa kushauri pale panapotakiwa badala ya kung’ang’ania uchawa (tabia ya kujipendekeza).

Mbunge wa Viti Maalum, Nusrat Hanje ameyasema hayo leo Mei 24, wakati akizungumza kuhusu mdahalo wa vijana utafanyika Mei 25, 2025 unaolenga kuzungumzia miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema pamoja na mambo mengine mdahalo huo utaweka viwango vya aina ya vijana wanaohitajika katika Tanzania.

“Tunahitaji vijana ambao wanaweza kujenga hoja, tunahitaji vijana wanaoweza kushauri, sifikirii hata hao viongozi wanataka vijana ambao sifia, sifia tu. Hata mheshimiwa Rais alisema tuikosoe Serikali kwa hoja,” amesema.

Amesema ni matumaini yake baada ya mkutano huo watakwenda kuwa na vijana wanaoweza kujenga Taifa na sio wabeba mikoba ya viongozi ama chawa ambao hawashauri panapohitajika.

“Isionekane kama ni uchawa mtu akiamua kuzungumzia vizuri kiongozi wake kama amefanya vitu vizuri. Mahali ambapo unatakiwa kushauri bado unasifia wakati mwingine labda mwenyewe amekwama anatakiwa kushauriwa lakini wewe unasifia. Tutajadili hilo,” amesema.

Kuhusu ushiriki wa vijana katika uchaguzi, Nusrat amesema ni katika mdahalo huo pia watajadili ushiriki wa vijana kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.

Amesema ni vyema vijana wakawania nafasi kuanzia katika Serikali za mitaa na vijiji hadi ngazi za kitaifa na kuwa vyama vya siasa vina jukumu la kuweka vijana chini ya miaka 35 kwenye teuzi za wagombea.

“Lakini bado kuna changamoto za kiuchumi kwa vijana chini ya miaka 35 hasa katika wabunge wanaume. Wao hawana nafasi viti maalum ni lazima ukagombee, kijana gani anaweza kuwa na uwezo wa kiuchumi kwenda kuchangia,” amesema.

Amesema hata kuendesha kampeni kunahitaji fedha lakini kijana huyo ndio kwanza ametoka chuo anajitafuta kiuchumi ili kupata fedha za vipaza sauti na magari ya kufanya kampeni.

Kwa upande wa mdahalo, Nusrat amesema mdahalo huo utahusisha makundi ya vijana kutoka jumuiya ya vyama vya siasa, asasi za kiraia, viongozi wa dini wote na wanafunzi kutoka taasisi mbalimbali za elimu.

Pia amesema wawakilishi wa wizara zinazojishughulisha na masuala ya vijana, watashiriki kwenye mdahalo huo na viongozi wa vijana kwenye vyama vya siasa vya CCM, ACT-Wazalendo, CUF na vingine.

Mkazi wa Nkuhungu Jumanne Swalehe, amesema changamoto za vijana ziko nyingi lakini ukosefu wa ajira ni tatizo kwa vijana wengi wanaomaliza elimu na mafunzo.

“Tunaomba Serikali ijizatiti katika kuongeza mikopo kwa vijana ili waweze kujiajiri kwenye shughuli mbalimbali kwa kuwa tatizo jingine ni ukosefu wa mitaji,” amesema.

Mwishoni mwa mwaka jana vilizuka vikundi kwenye maeneo mbalimbali  nchini vikijipachika kuwa ni chawa wa mama, jambo lililofanya kwa nyakati tofauti viongozi wa CCM kujitokeza hadharani na kupiga marufuku.

Agosti 7 mwaka jana Chama cha CCM Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam, kilipiga marufuku kundi la chama cha mama kikieleza dhamira yao ni kusaka madaraka.

Desemba 14, mwaka jana Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Dar es Salaam, Khadija Ally Said alikataa tabia ya makada wa chama hicho kusifiwa ovyo (uchawa).

“Nilisema mimi siyo mwenyekiti wa uchawa, wa kusifiwa, mimi ni mwenyekiti wa kazi, tunategemea katika nafasi zetu, tutakwenda kufanya kazi kubwa kama jumuiya ya wazazi katika elimu na malezi, tuna changamoto ya malezi,” alisema.

Related Posts