Dodoma. Baada ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kutangaza kuandikisha wafungwa wa chini ya miezi sita katika daftari la kudumu la wapigakura, wadau wametaka marekebisho ya sheria ili kuruhusu wafungwa wote kupiga kura kwa sababu maisha yao yanaathiriwa na wanasiasa.
Mei 11, 2024, wakati akizungumza Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Ramadhan Kailima, alisema wafungwa katika magereza au wanafunzi waliopo kwenye vyuo vya Mafunzo Zanzibar, watakaokuwa wamehukumiwa chini ya miezi sita na mahabusu wataandikishwa katika orodha ya wapigakura.
“Ukisoma ile Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, kifungu cha 42 kinatoa fursa hiyo, kwamba Tume inaweza kuweka utaratibu mtu akapigia kura popote pale nje ya eneo alipojiandikisha lakini sio kwa kura ya ubunge na udiwani.
Pia, alisema jambo jipya katika kanuni za uandishaji wapiga kura ni kuwa watu wanaotaka kuboresha taarifa zao katika daftari la wapiga kura wanaweza pia kutumia simu ya mkononi, kuipata huduma hiyo.
Amesema kwa mfumo huo, mtu atatakiwa kuwa na kadi yake ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA), wakati wa mchakato huo,hatua ambayo itapunguza msongamano.
Hata hivyo, mfumo huo hauwahusu wale wanaoanza kujiandisha katika daftari hilo.
Akizungumza na Mwananchi, Mchambuzi wa masuala ya siasa, Deus Kibamba, amesema kupiga kura ni sawa na uhai na ndio maana imewekwa katika Katiba kuwa miongoni mwa haki.
Amesema ingawa walishikilia kutaka wafungwa wapige kura wakati wa marekebisho ya sheria za uchaguzi, lakini waliwakubalia nusu kwa kuruhusu sehemu ya wafungwa.
Kibamba aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, ameipongeza Tume kwa kuanza utekelezaji mara moja wa sheria hiyo na kutaka kufanyika hivyo kwa sheria nyingine.
“Tumepiga hatua kwa kweli lakini ni nusu mkate, tunahitaji maboresho zaidi ya sheria ili wafungwa wote waweze kupiga kura.
Hata kama amefungwa maisha ama amehukumiwa kunyongwa, mimi maoni yangu bado anapaswa kupiga kura, kwa sababu naye maisha yake yanaathiriwa na wanasiasa,”amesema.
Kibamba amesema kupita kwa sheria ni mwanzo wa marekebisho ya sheria husika na sheria nyingine na hivyo anashauri yafanyike marekebisho ya sheria za uchaguzi ili kuruhusu wafungwa wote kupiga kura.
Amepongeza hatua ya kubadilisha kifungu cha sheria kinacholazimisha mkurungezi wa halmashauri kuwa msimamizi wa uchaguzi.
Hata hivyo, amesema huenda Bunge lilisahau kuacha kubadilisha kifungu kinachotamka kuwa mkurugenzi wa halmashauri ndiye msimamizi wa shughuli ya undikishaji wapiga kura.
“Ilikuwa wakurugenzi wasihusike katika mchakato wa uchaguzi kabisa. Sababu ya kuwakataa ambayo inafanya pia hata kuwakataa watumishi wa umma ni kwamba wakurugenzi na watumishi wa umma wameshindwa kuwa huru kujiepusha na siasa za vyama vya siasa,”amesema.
Amesema ni vyema wakurugenzi wakaondolewa katika usimamizi wa uandikishaji wapiga kura kwa sababu huo ndio mwanzo wa uchaguzi.
Aidha, amesema watalitaka sheria ilazimishe Tume kuandikisha kura kidijitali badala ya watu kuwasubiri waandikishaji wapiga kura wafike katika vituo vya uandikishaji, lengo likiwa ni kuondoa msongamano wa watu kwenye vituo vya upigaji kura.
Naye Mratibu wa Mtandao wa Haki za Binadamu (THRD) Onesmo Ole Ngurumwa, amesema kuwa mfungwa haiondoi haki ya kupiga kura kwa sababu bado anahudumiwa na viongozi wanaochaguliwa na wananchi.
“Mtu yeyote anayehudumiwa na viongozi wanaochaguliwa anapaswa kushiriki kuchagua viongozi.Mfungwa anahudumiwa na idara ambazo zinaongozwa na viongozi tuliowachagua, hivyo kwa hiyo anayo haki ya kuwachagua hata kama yuko gerezani,”amesema.
Amesema sheria haitakiwi kumzuia mtu yeyote aliyefungwa ama kutuhumiwa kupiga kura kwa sababu wote ni Watanzania.
Amesema hiyo ndiyo iliyosababisha waamue kufungua kesi mahakamani kudai wafungwa na watuhumiwa walio mahabusu kupiga kura.
Mwanasheria wa kujitegemea, Elias Machibya, amepongeza hatua ya Serikali kuruhusu wafungwa hao kupiga kura na kuwa ni mwendelezo wa kuimarisha haki za raia nchini.
“Najua Serikali inazo takwimu watu wangapi wapo magerezani wenye kifungo chini ya miezi sita ambao usipowaandikisha utakuwa umewanyima haki hiyo…Hiki ni kitu kizuri kinaendelea kuimarisha haki za raia katika nchi yetu,”amesema Machibya
Mei 11 mwaka huu, NEC ilipitisha Kanuni za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi za Mwaka 2024 na Kanuni za Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura za Mwaka 2024 ikiwa ni hatua ya kuzitafsiri sheria zilizotungwa na Bunge hivi karibuni.
Sheria zilizotungwa na Bunge zinazohusu uchaguzi ni Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2024 na Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya Mwaka 2024.
Hata hivyo wakati wa mijadala ya miswada ya sheria za uchaguzi Februari mwaka huu, Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), kiliamsha tena haja hiyo kwa kupendekeza wafungwa kupiga kura katika uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani.
Kabla ya hapo, Mahakama Kuu nchini wa Mei mwaka 2022, ilibatilisha kifungu cha 11(1) (c) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi na kuwapa haki wafungwa wa makosa ya kawaida ya jinai, kupiga kura katika uchaguzi Mkuu.
Msingi wa uamuzi wa mahakama hiyo ni kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na mwanaharakati, Tito Magoti na John Tulla ambao mwaka 2020 walikosa haki ya kupiga kura kwa kuwa walikuwa mahabusu.
Kabla ya uamuzi huo wa mahakama, kifungu hicho cha sheria hiyo ya uchaguzi, kilizuia wafungwa wanaotumikia adhabu ya kunyongwa na wale wa kifungo cha kuanzia miezi sita hawakuwa na haki ya kupiga kura.