Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande amepongeza Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa utendaji mzuri unaochangia katika kukuza maendeleo ya Taifa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma… (endelea).
Chande ametoa pongezi leo tarehe 20 Mei 2024 jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha Wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Akifafanua Chande amesema kuwa mafanikio ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo yanatokana na utendaji mzuri wa NBS kwa upande wa Tanzania Bara na OCGS kwa upande wa Zanzibar.
Mafanikio hayo ni pamoja na ujenzi wa majengo ya Ofisi hizo, Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Sensa ya Majengo, Sensa ya Anuani za Makazi na kufanyika kwa Sensa kwa njia ya kidijitali.
Chande amesema mafanikio hayo ni matokeo ya utashi wa kisiasa wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Awamu ya Nane Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Aidha, amewataka watumishi wa Ofisi hizo kufanya kazi kwa weledi na uadilifu ili kuongeza tija katika uzalishaji wa takwinu hapa nchini kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.
Naye, Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 Anne Makinda amesema kuwa Watakwimu wana mchango mkubwa katika kuchochea maendeleo ya taifa kwani mipango yote ya maendeleo inategemea takwimu.
Naye Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk. Albina Chuwa amesema kuwa kikao kazi hicho ni cha kihistoria tangu kuanzishwa kwa Ofisi hizo kwani kimewaleta pamoja watumishi wa pande zote mbili za Muungano.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi wa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Balozi Amina Salum amesema kuwa utamaduni wa watumishi wa Ofisi zote mbili kukutana kupitia kikao kazi unapaswa kuendelezwa.
Kikao Kazi cha watumishi wa NBS na OCGS kinafanyika jijini Dodoma Mei 20 – 21, 2024.