Zuma hastahili kugombea katika uchaguzi mkuu Afrika Kusini – DW – 20.05.2024

Mapema leo Mahakama ya kikatiba ya Afrika Kusini imetoa uamuzi kuwa rais wa zamani wa nchi hiyo Jacob Zuma hastahili kugombea katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu. Inaelezwa kwamba Uamuzi huo uliofuatiliwa kwa ukaribu na watu wengi nchini humo unaweza kuathiri matokeo ya uchaguzi ujao.

Soma zaidi. Zuma hapaswi kushiriki uchaguzi wa bunge

Kesi hiyo imetokana na uamuzi wa mwezi Machi uliotolewa na tume ya uchaguzi ya Afrika ya Kusini wa kutomuidhinisha Jacob Zuma kuwa mgombea katika uchaguzi mkuu na kwamba katiba ya Afrika ya Kusini inatoa katazo kwa mtu yeyote kugombea ikiwa amewahi kufungwa jela kwa zaidi ya mwaka mmoja au zaidi.

Mnamo 2021,Zuma alihukumiwa kifungo cha miezi 15 jela kwa kushindwa kufika mahakamani kujibu tuhuma zilizokuwa zikimkabili katika uchunguzi wa kesi ya rushwa.

 Jacob Zuma
Mwaka 2021 Jacob Zuma alihukumiwa kifungo cha miezi 15 kwa kushindwa kufika mahakamani kujibu tuhuma zilizokuwa zikimkabili katika uchunguzi wa kesi ya rushwaPicha: Kim Ludbrook/AFP/Getty Images

Mwezi April mwaka huu, mahakama ilibatilisha uamuzi huo na kusema kwamba kifungu husika cha katiba kinatumika tu watu waliokuwa na nafasi ya kukata rufaa dhidi ya hukumu zao na hivyo kesi ya Zuma haikuwa miongoni mwa kesi hizo.

Baada ya hapo tume ya uchaguzi ilipinga uamuzi huo katika mahakama ya katiba na leo imetoa uamuzi kwamba rais huyo wa zamani wa Afrika ya Kusini hastahili kugombea tena katika uchaguzi mkuu utakaofanyika wiki ijayo- Mei 29.

Soma zaidi. Zuma azindua ilani ya uchaguzi kwa kutoa ahadi lukuki

Wakati ikitoa uamuzi huo mahakama ya katiba ilisema na hapa nanukuu ” Inatangazwa kuwa Bwana Zuma alitiwa hatiani kwa kosa na kuhukumiwa kifungo cha zaidi ya miezi 12 na kwa mujibu wa katiba ni kwamba hastahili kugombea katika uchaguzi mkuu”mwisho wa kunukuu.

Zuma aliyekuwa rais wa Afrika Kusini kuanzia 2009-2018 alijiuzulu katika nafasi hiyo kwa tuhuma za ufisadi ingawa mwishoni mwa mwaka uliopita alirudi tena kwenye ulingo wa kisiasa akiwa na chama kipya cha MK na amekuwa akikosoa vikali chama chake cha zamani cha ANC ambacho amewahi kukiongoza.

 Jacob Zuma
Jacob Zuma akiwa mahakamaniPicha: Jerome Delay/AP/picture alliance

Nini kitatokea?

Hata hivyo, Wafuatiliaji wa siasa za Afrika ya Kusini wanahofu kwamba kukatazwa kwa Zuma kugombea katika uchaguzi mkuu nchini humo kunaweza kuathiri matokeo ya uchaguzi huo, ikumbukwe kuwa mwaka 2021 ilipotolewa hukumu ya kufungwa kwa Zuma kulizuka ghasia huko kwa Zulu Natal na zaidi ya watu 300 walipoteza maisha. 

Soma zaidi. Mahakama Afrika Kusini yasikiliza kesi ya Zuma kugombea urais

Mwishoni mwa juma, Zuma mwenyewe aliendelea na kampeni zake mjini Johannesburg ambapo maelfu ya wafuasi wake walikusanyika katika uwanja wa Orlando wakisikiliza sera zake na chama chake kipya cha MK.

Nini kitafuata baada ya kutolewa kwa uamuzi huu na mahakama ya kikatiba, ni jambo la kusubiri.

Mwandishi: Suleman Mwiru
Vyanzo: Reuters, AP na AFP

 

Related Posts