Mwanza. Mkazi wa Mtaa wa Nyakato wilayani Ilemela jijini hapa, Bashiri Mohamed (35) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Ilemela mkoani humo akikabiliwa na shtaka la kufanya ngono na binti yake mwenye umri wa miaka (16).
Bashiri amepandishwa kizimbani mahakamani hapo Leo Jumanne, Mei 21, 2024 na kusomewa shtaka hilo na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mwanahawa Changale, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Juma Opudo.
Akisoma mshtakiwa huyo shtaka hilo, Wakili Changale amesema kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo kati ya Septemba 2023 hadi Februari 15, 2024 kinyume na kifungu namba 158 (1) (a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Wakili Changale amesema kuwa katika kipindi hicho, mshtakiwa kwa tarehe tofauti eneo la Nyakato-Mecco ndani ya wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza alifanya ngono na binti yake huyo wa kumzaa (16) huku akitambua ni mtoto wake wa kumzaa.”
Hata hivyo mshtakiwa (Bashiri) ambaye anawakilishwa na wakili, Michael Mlekwa, amekana shtaka linalomkabili na kuiomba mahakama kumpatia dhamana kwani shtaka linalomkabili linadhaminika.
Mwendesha mashtaka huyo ameieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo ya jinai namba 13448/2024, umekamilika na akaiomba mahakama kupanga tarehe kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali ya kesi.
Hakimu Opudo amesema kuwa dhamana ya mshtakiwa huyo Iko wazi Kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili wenye Kitambulisho cha Utaifa (Nida) ama cha mpiga kura, watakaosaini Bondi ya dhamana ya Sh4 milioni kila mmoja.
Pia amemtaka mdhamini mmoja kuwa na mali isiyohamishika masharti ambayo mshtakiwa ameshindwa kutimiza kwani barua ya utambulisho ya mdhamini mmoja aliyetokea wilayani Magu mkoani humo imekosa uthibitisho wa Hakimu Mfawidhi wa Wilaya ya Magu na hivyo kukosa dhamana.
“Barua yako sitoipitisha kwa sababu unatokea wilaya nyingine na haijapitia kwa Hakimu Mfawidhi wa wilaya unayotoka. Kwa hiyo shauri lako litaitwa kesho kwa ajili ya kukamilisha mchakato wa dhamana”, amesema Hakimu Opudo, huku pia akipanga kesi hiyo kuendelea Juni 11, 2024 kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali.
Baada ya kushindwa kutimiza masharti hayo, mshtakiwa amerejeshwa rumande hadi atakapotimiza matakwa hayo.