Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Emmanuel Nchimbi, amewataka watumishi wanaosimamia utawala na rasilimali watu sehemu za kazi kuwatendea haki wafanyakazi wote kwa kujiepusha na vitendo vyovyote vya uonevu.
Akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya wataalam wa rasilimali watu na utawala duniani, jana Jumatatu, Mei 20, 2024, ambayo kitaifa imefanyika mkoani Morogoro, Balozi Nchimbi amewataka watumishi wanaosimamia rasilimali watu na utawala kujiepusha na uminyaji haki na badala yake wajali stahiki za wafanyakazi zilizopo kisheria.
“Dhamana ya nafasi zenu ni kusimamia utawala na rasilimali watu zitaendelea kuhitajika na kuheshimika iwapo baadhi ya watendaji wanaoendekeza tabia ya kujifanya ‘miungu watu’, na kuweka mbele maslahi binafsi katika ofisi wanazozisimamia, wataacha tabia hizo,”amesema.
Katibu Mkuu huyo wa CCM ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo, amewataka Wanachama wa Wanachama wa Chama cha Wataalamu wa Rasilimali Watu na Utawala Tanzania (THRAPA), kila mmoja wao kujiona ana deni la kutoa utumishi wa kusaidia wafanyakazi kupata haki na maslahi yao katika sehemu zao za kazi.
“Ni muhimu sana tukumbushane kuwa tuna dhima kubwa ya kusaidia kujenga na kuimarisha nguvu kazi endelevu katika maeneo yetu ya kazi na kwenye ofisi zetu. Taaluma yetu hii itaendelea kuhitajika na kuheshimiwa iwapo sote tutatimiza wajibu wetu wa kuhakikisha watu wanapata haki na maslahi yao.
Baadhi yetu waache kujifanya miungu watu, wanaonea watu na kutisha watu. Unakalia faili la mtu mwaka mzima. Tuache hizo tabia mbaya,” amesema.
“Watu wapande madaraja yao kwa sifa zao, wapate vyeo kwa sifa, wapate safari kwa sifa. Watu wapate madai yao, mishahara, posho, likizo…hizo zote ni haki za watu,” amesema.
Dk Nchimbi amesema:“Tusimamie haki za watu bila haya. Msionee watu wala kuleta undugu au kuomba rushwa ndiyo mtu apate haki na maslahi yake. Kila mmoja wetu atambue analo deni la kutumikia watu kwa kutanguliza maslahi ya taasisi na watu mbele, kuliko maslahi yake binafsi.”
Pia Dk Nchimbi Nchimbi amemwelekeza Waziri wa Nchi, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene kukutana na uongozi wa THRAPA ili kumaliza sintofahamu inayowakabili wataalamu wa utawala na rasilimali watu walioko katika sekta ya umma, ambao wamekuwa wakizuiwa na baadhi ya waajiri wao kushiriki shughuli au kuwa wanachama wa chama hicho.
Katika hatua nyingine, Dk Nchimbi amekubali ombi la wanachama wa THRAPA waliomtaka awe mlezi wao, huku pia akiunga mkono dhamira yao ya kutaka chama hicho kiwe na bodi ya kitaaluma kama zilivyo bodi za baadhi ya taaluma nyingine na kusisitiza kuwa katika jambo hilo CCM itakuwa nao bega kwa bega kulifanikisha.