Dodoma Jiji, Yanga vita iko hapa, Arajiga kati

KWA mashabiki wa Dodoma Jiji wanajiuliza kwanini timu hiyo kwanini haijafunga bao katika mechi nne mfululizo za Ligi Kuu Bara zilizopita wakati kesho itakapoikaribisha Yanga saa 10:00 jioni, Uwanja wa Jamhuri Dodoma.

Swali hilo linatokana na safu butu ya ushambuliaji inayoikumba timu hiyo ambapo katika michezo minne imeshindwa kabisa kufunga bao lolote tangu mara yake ya mwisho ilipoifunga KMC 1-0, Aprili 26, mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma.

Katika michezo hiyo minne, Dodoma ilianza kwa kichapo cha mabao 2-0, dhidi ya Singida Fountain Gate na kutoka suluhu mechi mbili mfululizo ikianza na Tanzania Prisons, Namungo kisha kuchapwa bao 1-0, mechi yake ya mwisho na Simba Mei 17.

Ukiachana na hilo ila jambo lingine ni kwamba katika wachezaji wanaoongoza kuifunga Yanga wa upande wa Dodoma Jiji ni aliyekuwa nyota wa kikosi hicho, Seif Karihe ambaye kwa sasa anakipiga katika timu ya Mtibwa Sugar ya mkoani Morogoro.

Iko hivi, tangu Dodoma Jiji ipande rasmi Ligi Kuu Bara msimu wa 2019/2020, imekutana na Yanga mara saba ambapo kati ya hiyo imefunga jumla ya mabao matatu huku mawili yakifungwa na Seif Karihe ambaye hata hivyo hayupo ndani ya timu hiyo.

Mchezo wa kwanza kwao kukutana katika Ligi Kuu Bara ulipigwa Desemba 19, 2020 na kuisha kwa ushindi wa mabao 3-1, huku Karihe akifunga dakika ya tatu tu kisha Lamine Moro, Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ na Bakari Mwamnyeto wakitupia kwa Yanga.

Karihe aliendeleza tena kisimati wakati timu hizo zilipokutana kwenye Uwanja wa Azam Complex ambapo alifunga bao moja wakati Yanga iliposhinda mabao 4-2, Mei 13, 2023, huku mchezo huo ukikumbukwa zaidi kwani ndio uliowapa ubingwa wa Ligi.

Katika mchezo huo, mabao ya Yanga yalifungwa na Kennedy Musonda, Mudathir Yahya, Farid Mussa na Fiston Mayele huku mbali na Karihe aliyefunga kwa Dodoma ila bao lingine lilifungwa na Collins Opare aliyeondoka na kujiunga na Al-Zawraa SC ya Iraq.

Hii ni mechi ambayo presha zaidi iko kwa Dodoma Jiji ambayo katika michezo 27 iliyocheza imeshinda saba, sare tisa na kupoteza 11 ikiwa nafasi ya 11 na pointi 30 sawa na Singida Fountain Gate ambazo zote haziko sehemu salama ya kubakia.

Pointi hizo zinaifanya kutokuwa kwenye wakati mzuri wa kujihakikishia kubaki tena katika Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao kwani zinaweza kufikiwa na timu zilizopo chini yake zikiwemo Geita Gold yenye 25 na Tabora United na Mashujaa zenye 26.

Yanga ambayo kwa sasa haina cha kupoteza baada ya kutetea taji lake inaingia katika mchezo huo ikiwa na matokeo mazuri ya hivi karibuni kwani mara ya mwisho kupoteza katika Ligi Kuu Bara ilikuwa mabao 2-1, dhidi ya Azam FC, Machi 17, mwaka huu.

Tangu timu hizi zilipoanza kukutana katika Ligi Kuu Bara ni mchezo mmoja tu kati ya saba ambao hazijafungana ila mingine yote mabao yamefungwa.

Mchezo ulioisha bila bao kwa maana ya kushindwa kufungana baina ya timu hizi ulipigwa Uwanja wa Jamhuri Dodoma Julai 18, 2021.

Katika michezo saba ya Ligi Kuu Bara timu hizo zilipokutana Yanga imekuwa mbabe zaidi kwani imefunga jumla ya mabao 16 wakati Dodoma imefunga matatu tu huku mechi iliyozalisha mabao mengi ni ile ya ushindi wa Yanga wa 4-2, Mei 13, mwaka jana.

Kwa maana hiyo Dodoma Jiji haijawahi kuifunga Yanga tangu zimeanza kukutana kwani mara ya mwisho zilikutana katika hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) ambapo ilichapwa pia mabao 2-0, Uwanja wa Jamhuri Aprili 10, mwaka huu.

Makocha wa timu zote watahitaji kupambana kwa ajili ya kuhakikisha wanapata matokeo chanya ingawa kazi kubwa itakuwa kwa Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji Mkenya, Francis Baraza tofauti na mwenzake Muargentina, Miguel Gamondi anayesaka heshima tu.

Baraza aliyeanza kukinoa kikosi hicho Desemba 16, mwaka jana akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Mmarekani, Melis Medo alisema kwake ni mechi ngumu japo timu hiyo imejipanga vyema kukabiliana na washindani wao ili kupata pointi zote tatu.

“Tunashukuru hali ya kikosi ni nzuri kwa sababu tangu mchezo wetu wa mwisho na Simba hakuna aliyekuwa majeruhi, kikubwa ninachopambana nacho ni kutengeneza saikolojia yao vizuri kwa sababu tunatengeneza nafasi ila hatuzitumii,” alisema.

Baraza ametoa nafasi kwa kila mchezaji ndani ya timu hiyo wakiwemo nyota wawili wapya Wakenya, Robinson Kamura (Kakamega Homeboyz) na Apollo Otieno aliyetokea KCB ambao wote wamekuwa muhimili kwenye eneo la ulinzi na kiungo wa ushambuliaji.

Nyota wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua amesema presha kubwa iko kwa Dodoma Jiji kutokana na nafasi iliyopo ingawa licha ya kutopata matokeo mazuri kwa mechi za hivi karibuni ila wameonyesha soka safi wanapocheza uwanja wao wa Jamhuri.

“Francis Baraza ameibadilisha sana Dodoma kiuchezaji kwa sababu unaona timu inacheza vizuri na kila mchezaji amempatia nafasi ya kucheza, hautokuwa mchezo mwepesi kwao kwani hakuna asiyejua ubora wa Yanga tangu msimu huu umeanza,” amesema.

Kwa upande wa Gamondi ambaye ni msimu wake wa kwanza akiwa na kikosi hicho na kuipa ubingwa wa Ligi Kuu Bara amesema licha ya mafanikio waliyofikia ya kutetea taji lao ila ametoa tahadhari kwa wachezaji kuendelea kupambana hadi mechi ya mwisho.

“Lengo letu lilikuwa kuchukua ubingwa na tumefanikiwa lakini bado tunahitaji kuhakikisha michezo yote iliyosalia sisi kama benchi la ufundi na wachezaji tunaendelea kuvuna pointi tatu, tuko makini na kila mpinzani aliyekuwa mbele yetu.”

Gamondi ameongeza hali ya wachezaji ni nzuri isipokuwa wataangalia utimamu wa beki wa kushoto wa timu hiyo, Nickson Kibabage ambaye alipata majeraha wakati wa mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Ihefu.

Muhimili mkubwa wa Dodoma ni eneo la kati linaloundwa na Salmin Hoza, Rajab Seif, Gustapha Saimon na Apollo Otieno ambao watakuwa na wakati mgumu wa kupambana na viungo wa Yanga wakiwemo, Khalid Aucho, Mudathir Yahya na Salum Abukabar ‘Sure Boy’.

Dodoma imekuwa haina safu bora ya ushambuliaji na kwa kuthibitisha hilo katika michezo 27 iliyocheza imefunga jumla ya mabao 17 tu ikiwa ni timu ya pili inayoongoza kwa kufunga idadi ndogo nyuma ya Geita Gold inayoshikilia usukani na 16.

Nyota anayeongoza kwa kufunga ndani ya kikosi hicho ni Hassan Mwaterema mwenye mabao manne ambaye naye mechi ya mwisho kufunga ilikuwa ya ushindi wa timu hiyo wa bao 1-0, dhidi ya Tabora United Machi 6, mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri.

Mastaa wengine wanaofuatia kwa Dodoma ni Emmanuel Martin na Paul Peter ambao kila mmoja wao amefunga mabao matatu ya Ligi Kuu Bara.

Wakati Dodoma ikiwa na safu butu, hali ni tofauti kwa upande wa Yanga kwani ndio inayoongoza kwa kufunga idadi kubwa ya mabao ikiwa imefunga 60 hadi sasa nyuma ya Azam FC iliyopo ya pili iliyofunga 54 na Simba inayoshika ya tatu na 52.

Nyota tishio ndani ya kikosi cha Yanga msimu huu ni Stephane Aziz KI ambaye hadi sasa anaongoza kwenye vita ya ufungaji bora akiwa amefunga mabao 15 sawa na kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyefunga pia idadi kama hiyo.

Wengine wanaofuatia kwa ufungaji ndani ya Yanga ni Mudathir Yahya na Maxi Mpia Nzengeli ambao kila mmoja wao amefunga mabao tisa huku mshambuliaji wa kikosi hicho, Joseph Guede akiwa kwenye kiwango bora akiwa amefunga matano hadi sasa.

Katika mchezo huu wachezaji wa Dodoma watatangulia kutoka vyumbani na kupanga mstari kabla ya mechi kuanza kama ishara ya kuwapigia makofi nyota wa Yanga watakapotoka kutokana na kutwaa ubingwa wao wa Ligi Kuu Bara ikiwa ndio utaratibu.

Yanga ilitangazwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya ushindi wa mabao 3-1, dhidi ya Mtibwa Sugar Mei 13, mwaka huu kufuatia kufikisha jumla ya pointi 71 ambazo hazitafikiwa na timu yoyote kati ya 16 zinazoshiriki.

Mwamuzi wa kati wa mchezo huu atakuwa ni Ahmed Arajiga kutoka Manyara akisaidiwa na mwamuzi namba moja, Hamdan Said wa Mtwara na mwamuzi msaidizi namba mbili, Arnold Bugado (Tanga) wakati mwamuzi wa akiba ni Charles Simon kutokea Dodoma.

Rekodi zinaonyesha michezo mitano ambayo Arajiga ameichezesha Yanga msimu huu katika Ligi Kuu Bara timu hiyo haijawahi kupoteza.

Mchezo wa kwanza kwa Arajiga kuichezesha Yanga ulikuwa wa ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya JKT Tanzania (Agosti 29, 2023), ukafuata wa 3-2, mbele ya Azam FC (Oktoba 23, 2023), (5-1) v Simba (Novemba 5, 2023), (2-1) v TZ Prisons (Februari 11, 2024).

Baada ya hapo, akachezesha tena ‘Dabi ya Kariakoo’ ambayo Yanga ilishinda dhidi ya Simba kwa mabao 2-1, Aprili 20, mwaka huu.

Related Posts