EALA waanza uchunguzi dhidi ya Dk Mathuki

Arusha. Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wanatarajiwa kukutana hivi karibuni ambapo pamoja na mambo mengine watamthibitisha katibu mkuu mpya wa Jumuiya hiyo Caroline Mwende Mueke.

Serikali ya Kenya ilimpendekeza Caroline kuchukua nafasi ya Dk Peter Mathuki kwa miaka miwili iliyobaki, baada ya Dk Mathuki kuteuliwa kuwa Balozi wa Kenya nchini Russia na Rais William Ruto.

Iwapo uteuzi Caroline utathibitishwa, atakuwa katibu mkuu wa kwanza wa EAC kuondoka katika wadhifa huo kabla ya kumaliza muda wake wa miaka mitano.

Dk Mathuki aliteuliwa kushika wadhifa huo  Februari 27, 2021 wakati wa mkutano wa kwanza wa wakuu wa nchi uliofanyika kwa njia ya mtandao  kwa sababu ya mlipuko wa ugonjwa wa Uviko – 19.

Wakati Caroline akisubiri kuthibitishwa, Kamati ya Sheria, Haki na Hadhi za wabunge wa EALA, imeanza uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili , Dk Mathuki, ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka na kusababisha upotevu wa Dola za Marekani milioni sita.

Kwa mujibu wa chanzo cha uhakika kutoka EAC kimeieleza Mwananchi Digital leo Jumanne, Mei 21, 2024, kuwa wakuu wa nchi hizo wanatarajia kukutana muda wowote kuanzia sasa na miongoni mwa masuala watakayoyafanya ni pamoja na kumthibitisha katibu mkuu mpya atakayeteuliwa.

Kwa mujibu wa mkataba wa EAC, katibu mkuu anateuliwa na wakuu wa nchi na atahudumu kwa muda wa miaka mitano ambayo haiongezwi.

Aidha, katibu mkuu siyo kiongozi wa sekretarieti ya EAC, chombo cha utendaji wa Jumuiya lakini pia ni ofisa mkuu wa hesabu wa chombo hicho cha kikanda.

Vuguvugu la kuondolewa kwa Dk Mathuki kabla ya uteuzi mpya lilianzia kwenye kikao cha Bunge la Eala la Machi mwaka huu kilichofanyika jijini Nairobi, Kenya.

 Tuhuma hizo ziliibuliwa na kuwasilishwa na mbunge wa bunge hilo kutoka Sudan Kusini, Kennedy Mukulia.

Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni jijini Arusha, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Amashaka Ngole, alieleza kuwa baada ya kusikiliza tuhuma hizo, kamati hiyo inatarajia kumuita Dk Mathuki kujibu.

Alitaja tuhuma zinazomkabili Dk Mathuki kuwa ni  matumizi mabaya ya madaraka ikiwemo upotevu wa fedha za mfuko wa usalama ,uuzwaji wa mali za Jumuiya kwa bei ya hasara yakiwemo magari bila kufuata sheria, kuajiri wafanyakazi bila kushirikisha ofisi inayohusika na ajira , kuhamisha wafanyakazi, kuajiri walinzi na kufungua akaunti za fedha bila kufuata utaratibu.

“Tuhuma hizo ziliibuliwa nchini Kenya wakati wa kikao cha bunge letu lilipokuwa linajadili matumizi ya Dola za Marekani  milioni sita ambazo zinadaiwa kutumika bila kupata kibali cha bunge la EALA chini ya Katibu Mkuu huyo,” alisema.

Alisema kamati hiyo imekutana jijini Arusha ili kupitia nyaraka za ushahidi wa tuhuma hizo pamoja na kukusanya mashahidi na kuwahoji ili kupata uthibitisho wa kina, na baada ya hapo watamuita Dk Mathuki na kumhoji juu ya tuhuma hizo zinazomkabili.

Ngole alisema kamati ikikamilisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili Katibu Mkuu huyo, itawasilisha ripoti yake katika bunge la EALA linalotarajiwa kuketi Juni mwaka huu.

Dk Mathuki amewahi kuwa mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala) kwa kipindi kimoja cha miaka mitano na baadaye kuwa ofisa mtendaji mkuu wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) lenye makao makuu yake jijini Arusha.

Waliowahi kushika wadhifa huo ni Francis Muthaura (Kenya), mwaka 1996 hadi 2001,Nuwe Amanya Mushega (Uganda) mwaka 2001 hadi 2006, Balozi Juma Mwapachu wa Tanzania (2006-2011), Dk Richard Sezibera wa Rwanda (2011 hadi 2016) na Balozi Mfumukeko kuanzia Aprili 2016 hadi 2021.

Benki ya Dunia (WB) ilimteua kuwa mwakilishi wa mfuko wa nchi wakopaji na mwenyekiti mwenza kundi la nchi 22 za Afrika zikiwemo za EAC.

Kwa mujibu wa itifaki ya EAC, mkuu wa nchi anayestahili, anamteua mtu wa kujaza nafasi hiyo ambaye anapitishwa na mkutano wa wakuu wa nchi.

Wadhifa huo wa kawaida huwa wa mzunguko miongoni mwa nchi wanachama wanaoteuliwa huhudumu kwa miaka mitano.

Caroline ambaye ni mtaalamu wa sera za umma amefanya kazi katika mashirika na misheni mbalimbali za Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia elimu, sayansi na utamaduni (Unesco), Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) na Misheni ya Kulinda Amani ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini.

Related Posts