Fei Toto amwacha Azizi Ki, Kagera yapigwa nyumbani

Timu ya Azam FC, imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya JKT Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamhyo, Mbweni, Dar es Salaam.

Mabao ya mchezo huo yamefungwa na mshambuliaji Abdul Suleiman ‘Sopu’ dakika ya 30, huku Feisal Salum ‘Fei Toto’ akipiga msumari wa mwisho dakika ya 90.

Azam ambayo inagombea nafasi ya pili katika msimamo wa ligi imefikisha pointi 63 baada ya michezo 28, pointi tatu mbele ya Simba ambayo inacheza baadaye dhidi ya Geita Gold kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Fei Toto amezidi kukinyemelea kiatu cha ufungaji bora baada ya kufunga bao la 16 na kumzidi Stephane Aziz KI wa Yanga mwenye 15.

Mchezo mwingine uliochezwa kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba ulishuhudia Kagera Sugar ikikubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Coasta Union ambayo inaendelea kujiweka vizuri kwenye nafasi ya nne ya msimamo ikiwa na pointi 41 kwenye mechi 28, huku Kagera ikiendelea kusalia nafasi ya 10 ikiwa na pointi 31 kwenye mechi 28.

Mabao ya Coastal Union yamefungwa na Shedrack Mulingwe dakika ya 16 pamoja na Denis Modzaka aliyefunga la pili dakika ya 69, ilihali bao la kufutia machozi la Kagera limefungwa na Mbaraka Yusuphu dakika ya 73.

Related Posts