Lushoto. Frateri wa Kanisa Katoliki Shirika la Roho Mtakatifu Jimboni Tanga, Rogassion Hugho, anadaiwa kujinyonga hadi kufa.
Hili ni tukio la pili kwa viongozi wa dini kudaiwa kujinyonga. Mei 16, 2024 mkoani Dodoma, Askofu Mkuu wa Makanisa ya Methodist, Joseph Bundala naye alidaiwa kujinyonga ndani ya ofisi yake iliyopo katika kanisa hilo eneo la Meriwa jijini Dodoma.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana Jumatatu Mei 20, 2024 usiku, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi kuhusiana na kujinyonga kwa Frateli Hugho, amesema amekutwa amejinyonga kwenye nyumba yao ya Malezi ya Magamba aliyokuwa akiishi.
Hata hivyo, kamanda huyo amesema chanzo cha kujinyonga kwake kinadaiwa ni kufeli mtihani wake uliokuwa unampeleka kwenye daraja la upadri.
“Taarifa za awali tulizozipata zinadai sababu ya kujinyonga kwa mwanafunzi (Frateri) huyo, walikuwa na mitihani ya kuvuka kutoka ngazi moja, kwenda mwaka mwingine, sasa katika wenzake wote yeye peke yake ndio amefeli.
Hivyo kutokana na msongo wa mawazo ndiyo akafikia uamuzi huo wa kujinyonga,” amedai Kamanda Mchunguzi.
Amesema Polisi wanaendelea na uchunguzi wa kifo hicho na ukikamilika, taarifa kwa umma itatolewa.
Mwananchi leo Jumanne Mei 21, 2024, limezungumza pia na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Magamba wilayani Lushoto, Julias Nyangusi amesema tukio hilo lilitokea jana na taarifa za kujinyonga kwa Frateli huyo walizipata mchana.
Amekiri kuwa Hugho alikuwa akiishi kwenye nyumba ya malezi (wamezoea kuita chuo cha mapadri) iliyoko katika mtaa huo.
“Na taarifa za awali tulizozipata zinadai ni barua aliyopewa na uongozi wao ikimtaka aondoke kwenye nyumba hiyo kwa sababu hataweza kuweka nadhiri ya kiapo cha upadri mwezi ujao,” amedai mwenyekiti huyo.
Mwenyekiti huyo amedai taarifa zaidi zinadai marehemu ameacha ujumbe wa maandishi kwenda kwa mama yake unaosomeka; “Mama usilie, nimeshindwa kufikia malengo, ninajua nimewakwaza wengi,” amedai Nyangusi.
Mwananchi limewatafuta viongozi wa nyumba hiyo ya malezi na wengine wa Kanisa katoliki Jimbo la Tanga bila mafanikio.
Hata hivyo, mmoja wa viongozi wa nyumba hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa kuwa si msemaji, amesema ni kweli Fratel Hugho amejinyonga lakini ni mapema mno kuzungumzia hilo bali taarifa kamili zitatolewa na viongozi wa kanisa baadaye.
Endelea kutufuatilia pamoja na mitandao yetu kwa habari zaidi.