Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti amesema taarifa ya sampuli ya sensa ya kilimo, mifugo na uvuvi iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mwaka 2020, ilikadiriwa Tanzania inao mbwa 2,776,918. Anaripoti Mwandishi Wetu… (endelea).
Aidha, kupitia taarifa hiyo amesema mikoa iliyoongoza kwa mbwa wengi ni Geita (302,879), Mwanza (287,270) na Tabora (243,768).
Mnyeti amebainisha hayo leo Jumanne wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Yustina Rahhi aliyetaka kufahamu Tanzania inao mbwa wangapi, pia alihoji mipango ya serikali kudhibiti kichaa cha mbwa.
Akijibu maswali hayo, Mnyeti amesema wizara itaendelea kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu katika kuhakikisha takwimu sahihi za mifugo ikiwemo mbwa zinapatikana kwa wakati ili kuwezesha mipango ya Serikali ya kuendeleza Sekta ya Mifugo.
Akizungumzia kuhusu kichaa cha mbwa, Mnyeti amesema Serikali imeruhusu wadau kutoka sekta binafsi kutoa huduma ya kuchanja mbwa.
“Rai kwa wadau kuendelea kuchanja kwa wakati kwa sababu mbwa akishaumwa hatuna mbadala mwingine zaidi ya kumuondoa duniani,” amesema.