Mwananchi, La Liga watia nguvu Umitashumta 

KATIKA dhana ya kuwezesha jamii, Kampuni ya Mwananchi Communications (MCL) kwa kushirikiana na Ligi Kuu Hispania (La Liga) wamechangia vifaa vya michezo katika Wilaya ya Ubungo, Dar es Saalam kwa ajili ya mashindano ya  Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (Umitashumta) yanayoendelea kwenye Uwanja wa Kinesi.

Mbele ya mamia ya wanafunzi, Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Bakari Machumu na Mkuu wa Biashara Kwa Afrika wa La Liga, Jorge Gazapo Diez wamekabidhi vifaa hivyo leo na kueleza namna ambavyo wanajisikia fahari kwa taasisi hizo kuwa sehemu ya kuibua wachezaji wengine nyota kama vile Mbwana Samatta kutoka ngazi ya chini. 

Vifaa ambavyo vimetolewa ni jezi, skafu, bukta, kofia, mabegi, viatu na mipira kwa ajili ya michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu kwa wanaume na wanawake, riadha na fani za ndani kama vile kucheza ngoma.

Mashindano hayo ambayo yanalenga kuibua na kuendeleza vipaji vya wanafunzi kila mwaka huendeshwa kwa mfumo wa kanda ambapo wanafunzi wa shule za msingi huchujwa kuanzia ngazi ya shule, kata, tarafa, wilaya, mkoa hadi taifa na kuunda timu.

Wanafunzi wa kanda nne za wilaya hiyo ambazo ni Kibamba, Mbezi, Mburahati na Ubungo walikutana katika viwanja hivyo kwa ajili ya mchujo ambao utatoa wawakilishi 120 kwa ajili ya kuunda timu ya wilaya ambayo itaingia kambini Mei 26 kwenye Shule ya Mount Calverley Kibamba. 

Akizungumza katika hafla hiyo, Machumu amesema: “Mwananchi tumekuwa na uhusiano na ushirikiano mzuri na La Liga, hivyo tukaona ngoma ianzie nyumbani (Ubungo). Tukaona tutoe mchango kidogo kwa wilaya yetu kwa ajili ya kutengeneza kina Samatta (Mbwana) wengine. Hawaji kama uyoga wanatengenezwa kwa kuwa na vifaa sahihi na walimu”

“Kwanini tuna dhima inayosema tunawezesha Taifa. Kupitia gazeti la Mwanaspoti tumekuwa sokoni kwa zaidi ya miaka 20, tunaangalia sio tu kuripoti michezo, bali tunawezaje kuchochea uwekezaji katika michezo kupitia mchango kidogo ambao tunatoa ni kwa sehemu tu kwa ajili ya kuwezesha.” 

Machumu ameongeza kuwa, “gazeti la Mwanaspoti ni kubwa kuliko yote, maana yake ni nini. Maana yake ni kwamba mashindano ya Umitashuta yataonekana katika gazeti la Mwanaspoti na hapa ninapozungumza nipo na waandishi waandamizi kwa ajili ya kuripoti. Itatoka Ubungo na kusikia kwingine, shindaneni na sisi (pamoja na La Liga) tupo kwa ajili ya kuwasapoti.” 

Kwa upande wake, Jorge amesema La Liga itaendelea kushirikiana na Mwanaspoti kuhakikisha kwamba jamii inanufaika na kile ilicho nacho.

“Asanteni sana kwa kuwa hapa (wanafunzi). Hatukutaka kupoteza hii nafasi kwa kujumuika na Mwanaspoti ndio maana tulikubali mara moja wito (wa kujaa),” amesema.

Naye Ofisa michezo wa Manispaa ya Ubungo, Wikansia Mwanga ameishukuru Mwananchi na La Liga kwa kujitoa kuwashika mkono, huku akiahidi kwamba vifaa hivyo vitatumika vizuri kwa ajili ya kukuza na kuendeleza michezo wilayani humo.

Related Posts