MZEE WA KALIUA: Simba inahitaji watu wawili tu

MOJAWAPO kati ya semi za Kiafrika ni ile inayosema kwamba “kama unataka kwenda mbali, nenda na wenzako na kama unataka kwenda haraka, nenda peke yako.”

Huu ni wakati wa Klabu ya Simba kwenda haraka. Ni wakati wa kupunguza idadi ya watu wanaofanya uamuzi. Ni muda wa kuwa na wafanya uamuzi wachache. Mambo ya kamati nyingi umepitwa na wakati. Mambo ya kutegemea Friends of Simba kwenye uamuzi umeisha. Simba haihitaji tena Friends of Simba kutwaa ubingwa.

Simba inahitaji kuwa na mwekezaji na mtendaji mkuu kwenye kufanya uamuzi kwa maslahi ya klabu. Ukishapunguza watu wengi kwenye kufanya uamuzi unaleta wepesi kwenye taasisi. Watu wengi wanapaswa kuwa watekelezaji wa maono ya wachache. Watu wengi wanapaswa kuajiriwa ili kupokea maelekezo ya namna klabu inavyotaka kutekeleza malengo yake. Simba kwa sasa inahitaji watu wachache sana kwenye kufanya uamuzi. Sio kwamba Friends of Simba na makundi mengine hayafai, hapana. Ni watu wametoka na klabu tangu enzi na enzi, lakini zama zinabadilika. Hakuna klabu ya kisasa inayoongozwa na kamati. Hakuna. Zama zimebadilika watu wanaajiri wataalamu kwenye kila idara ili kujiendesha kibiashara. Muda wa klabu za soka kuendeshwa na makundi ya wanachama umepitwa na wakati. Watu wachache ndani ya klabu wanapaswa kufanya uamuzi, na waliobaki ni kupokea maelekezo ya utekelezaji. Kamati za ufundi kama za usajili, kamati za hamasa ni mambo tu ya kizamani. Muda wake umepita. Simba inahitaji tajiri mmoja na mtendaji mkuu mmoja mbeba maono. Wengine wanapaswa kuwa wapokea maelekezo na kwenda kuyatekeleza. Zama zimebadilika. Makundi yalikuwa na msaada mkubwa sana enzi za Mwalimu, lakini kwa sasa unahitaji watu wachache wenye uwezo wa kufanya maamuzi kwa niaba ya nashabiki na wanachama.

Ukitazama pale Yanga, kuna watu wawili tu wanaofanya uamuzi. Ni Hersi Said na Ghalib Said Mohammed. Ni tajiri na mtendaji mkuu. Sio kwamba Yanga haikuwa na makundi yenye nguvu. Sio kwamba Hersi na GSM wameyafukuza hayo makundi. Hapana. Uamuzi unafanywa na watu wachache ila utekelezaji unafanywa na watu wengi. Sio kwamba Yanga hakuna wazee. Wapo mpaka kesho, lakini sio sehemu ya uamuzi wa klabu.

Pale Yanga kuna watekelezaji wengi sana wa maono, lakini wanaofanya uamuzi ni wachache. Simba inapaswa nayo kubadilika. Zama zinasonga mbele. Ukishakuwa na wafanya uamuzi wengi ni ngumu kusogea  zama hizi.

Hakuna asiyejua pamoja na yote, lakini zama za tajiri Mohammed Dewji na mtendaji mkuu Barbara Gonzalez mambo yalikwenda. Barbara alikuwa mstari wa mbele kwenye kila kitu. Tajiri aliwezesha kila kitu na mambo yalikuwa safi. Sio kwamba Barbara alifanya kila kitu mwenyewe, hapana. Alikuwa na watekelezaji wa maono ya taasisi wengi. Moja ya kitu kinachokosekana pale Simba klabu inaishi kwa zama za zamani. Simba wanahitaji wafanya uamuzi wachache wa kisasa. Ni kweli klabu zetu bado hazijakamilisha mfumo wa uwekezaji kwa hiyo kuwa na tajiri mfia timu bado haiepukiki.

Moja kati ya maeneo ambayo Simba bado inayumba ni eneo la usajili. Bado kuna usajili unafanyika kizamani.

Pamoja na maendeleo ya teknolojia bado wenzetu wanamfuatilia sana mchezaji kabla ya kumsajili. Wachezaji wengi wanasajiliwa ligi zikiwa zinaendelea. Pata muda wa kumuona uwanjani hata zaidi ya mara tatu kabla ya kumsaini. Ni kweli hakuna anayepatia kila siku kwenye usajili, lakini huwezi kukosea kila siku. Mfumo wa upatikanaji wa wachezaji pale Simba unatia mashaka kidogo. Misimu mitatu ya hivi karibu Simba imekosea zaidi kwenye usajili kuliko kupatia. Wachezaji wengi wamekuwa wa kawaida. Wameshindwa kuleta utofuati kikosini. Simba inahitaji mtu mwenye jicho la wachezaji. Simba inahitaji timu ya kuangalia hao wachezaji kisha kuwa na watu wachache wenye kufanya uamuzi. Mambo ya kila kikundi kuleta wachezaji wao ni ya kizamani.

Timu zetu zimewahi kufanya hivyo mara nyingi nadhani inatosha. Simba inahitaji ile kombinesheni ya Mohammed Dewji na Barbara Gonzalez. Simba inahitaji kuja na kombinesheni kama ya GSM na Hersi. Wengine wabaki kuwa watekelezaji tu. Mambo ya klabu kubwa kuendeshwa na kamati imepitwa na wakati. Simba inahitaji watu wawili tu wa maana. Wengine wabaki kuwa watekelezaji wa maono ya klabu.

Kwa sababu mfumo wa uwekezaji haujakamilika ni lazima Simba iwe na tajiri mtoa pesa na mtendaji mkuu wa kisasa. Mpira bila pesa kwa zama hizi huwezi kutoboa. Uamuzi ni lazima ufanywe na watu wachache. Makundi ya klabu ya Simba kuna muda yanaiumiza Simba yenyewe. Wengine wabaki tu kuwa mashabiki. Kama Mohammed Dewji hatoi pesa ni heri kuachana naye. Kama anatoa pesa za usajili na uendeshaji aungwe mkono. Simba inahitaji watu wachache wa kufanya uamuzi. Simba inahitaji kupata watu wachache wenye jicho la usajili kuisuka upya timu ya ushindi. Hersi Said amekuwa fundi sana kuleta wachezaji. Anaweza kupoteza hata wachezaji watano bora msimu huu na asipate tabu msimu ujao. Anajipa muda wa kutosha wakati wa usajili kabla ya kufanya uamuzi. Sio kwamba anapatia kila siku lakini walau anapatia zaidi siku hizi kuliko kukosea. Simba inapaswa kuimarika zaidi eneo hilo. Kama MO anatoa pesa za usajili na hakuna mtu mwenye jicho sahihi la usajili ni kazi bure. Simba inahitaji watu wawili tu. Tajiri asiye bahiri na mtendaji mkuu mwenye kuijua dunia ya kisasa.

Mambo ya kuunda kamati ya kuifunga Yanga yamepitwa na wakati. Mambo ya kuona kuifunga Yanga ndiyo mafanikio ni mambo ya kizamani. Mambo ya kuendesha klabu kwa kutegemea kamati ni mambo pia ya kizamani. Uamuzi wa klabu ufanywe na watu wachache, wengine wabaki kuwa mashabiki.

Simba inakosa kombinesheni ya Barbara na Mohamed Dewji. Simba inarudi nyuma badala ya kwenda mbele. Kukosa ubingwa kwa msimu wa tatu mfululizo siyo dhambi, lakini lazima Simba ijifunze maisha ya zama mpya. Mambo yanabadilika. Jicho la kupata wachezaji bora pale Simba linapotea.

Simba inahitaji watu wawili kwenye kufanya uamuzi wengine wabaki kuwa watekelezaji. Namisi sana muunganiko wa Barbara na MO.

Related Posts