NAIBU WAZIRI SILINDE ATOA TAMKO WENYE MADENI YA CHAI

NAIBU Waziri wa Kilimo, David Silinde ameagiza wamiliki wa viwanda mbalimbali nchini vya chai kuhakikisha wanalipa madeni ya wakulima wa chai na Bodi ya Chai Tanzania itoe ripoti serikalini namna ambavyo malipo hayo yatafanyika ifikapo Juni mwaka huu.

Silinde pia amesema wizara hiyo inataka inajenga viwanda saba vipya vya chai nchini kwa lengo la kuondoa ukiritimba ambao umekuwa ukimuumiza mkulima kwa kuuza kwa bei ndogo na viwanda hivyo vimilikiwe na wakulima wadogo nchini.

Naibu Waziri Silinde, ametoa agizo hilo Jijini Dodoma wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Chai Duniani inayofanyika kimataifa kila mwaka Mei 21.

“Wenye viwanda vya chai ambao wanadaiwa na wakulima wahakikishe wanawalipa wakulima hadi kufikia Juni 2024, bodi iwasilishe taarifa ya malipo na hatua ambayo itachukua kwa wakulima,” amesema.

Pia aliagiza, wamiliki wa mashamba ya Kilolo wanatakiwa kuacha uchomaji mkaa kwenye mashamba kwani kufanya hivyo wanaharibu rutuba. Pia aliwataka wananchi walioingia mkataba wa kulima wa mashamba hayo yaliyofufuliwa na serikali, wanatakiwa kutekeleza mkataba huo ndani ya mwaka mmoja vinginevyo watanyang’anwa.

Bodi ya Chai inatakiwa kufuatilia wamiliki wa viwanda ambao havifanyi kazi na waandae ripoti ya utendaji wa viwanda vyao kwa lengo la kujua kama vinaongeza tija, ubora na kuongeza kasi ya uzalishaji chai nchini.

Wawekezaji wanatakiwa kuwekeza katika sekta ya chai kwa kuleta teknojia na mitaji mipya ili kuwezesha chai bora kuzalishwa kwa wingi na kuwa yenye ushindani kwenye soko la kimataifa.

Wamiliki wa viwanda vya chai nchini wanatakiwa kuuza walau asilimia 15 chai kwenye mnada wa Dar er Salaam uliozinduliwa Desemba mwaka jana na unafanyika kila Jumatatu.

Silinde alisema, serikali imetoa msukumo mkubwa kwenye sekta hiyo, kwa kuongeza bajeti 2020/21 kutoka bil 294 hadi sh trilioni 1.12 mwaka 2024/25. Pia kutoa ruzuku kwenye pembejeo ikiwemo mbolea, viuatilifu na miche bora kwa lengo la kuwezesha wakulima wadogo kuzalisha miche bora.

“Kipaumbele cha wizara ni kujenga viwanda saba vipya lengo kuhakikisha kuondoa ukiritimba ukimuumiza mkulima Korogwe, vimilikiwe na wakulima wadogo ni maelekezo ya Rais kuhakikisha yanafika kwa wananchi,” alisema.

Serikali imedhamiria kufufua mashamba yaliyokufa ya chai na mapya mfano la Kilolo kuongeza tija uzalishaji wa chai na kujenga miundombinu ya umwagiliaji, kwa Tume ya Umwagiliaji kuongezewa fedha kutoka Sh bil 45 sasa kufikia bilioni 400 ili kuwapa fursa wakulima wadogo, kati na wakubwa kulima misimu zaidi ya miwili.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Chai Tanzania, Mustapha Umande amesema wa Chai Wakulima wa Chai Duniani wanakusudia kuanzisha Taasisi ya pamoja inayoitwa INDO-AFRICA TEA ASSOCIATION ambayo itakuwa sauti ya pamoja ya wazalishaji chai duniani.

Umande amesema mazungumzo kwa ajili ya kuunda taasisi hiyo yataanza mwezi Juni, hivyo akaomba serikali kuwapa vibali kwenda kujadili kuanzisha chombo hicho.

“Chombo hicho kitafanana na OPEC ambayo wazalishaji wa mafuta wanasauti ya pamoja, vivyo hivyo wazalishaji wa chai watakuwa na sauti ya pamoja,” alisema.

Chai inazalishwa kwa wingi duniani kuna ziada ya kilo zaidi ya milioni 400 hivyo, baadhi ya nchi zilishauri kilimo hicho kisimame kwani kinasaidia wakulima zaidi ya 30,000 nchini na fedha kwani asilimia 80 ya chai inauzwa nje.

Katika miaka mitatu iliyopita zao limepata changamoto nyingi ikiwemo ya kushuka bei kuliko miaka 40 iliyopita, lakini Tanzania ikatetea kwamba kilimo cha chai kiendelee kulimwa kwani ni chanzo cha kipato kila mwezi, ajira na kiafya na inakua kutokana kwa kwamba kuna ardhi ipo, nguvu kazi na kupanua kilimo kama Kenya na India.

Kutokana na chai kuwa kinywaji cha pili, kutoka maji wazalishaji na wauzaji wa chai ambao wengi wapo katika nchi za Afrika Mashariki na India wakati watumiaji wapo urusi, mashariki ya kati pamoja na Ulaya ambao ndio wamekuwa wakipanga bei.

Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Chai Tanzania, Rukia Mwango alisema bodi hiyo inafanya kazi ya huduma za udhibiti katika tasnia ya chai, kuhamasisha mnyororo wa thamani, mkulima, mchakati kiwandani, mfungashaji, mfanyabiashara hadi kwa mnywaji wa chai, inahamasisha kutoa huduma bora ambayo mhusika anatarajia.
 

 NAIBU Waziri wa Kilimo, David Silinde akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya chai Duniani yaliyofanyika Leo Mei 21,2024 Jijini Dodoma huku akisisitiza kuwa Wizara ya Kilimo itajenga Viwanda saba vya chai ili kuondoa ukiritimba ambao umekuwa ukiwaumiza Wakulima wengi
 

Naibu Waziri wa Kilimo David Silinde  akikagua mazao ya Chai alipohudhuria kwenye siku ya maadhimisho ya chai Duniani iliyofanyika Leo Mei 21,2024 Jijini  Dodoma

 Meneja Mipango wa Bodi ya Chai Tanzania Rukia Muwango akiongea jambo wakati alipomuwakilisha Mkurugenzi wa Bodi ya Chai wakati wa maadhimisho ya siku ya Chai Duniani yaliyofanyika Leo Mei 21,2024 Jijini Dodoma

Related Posts