NYOTA wa Tanzania, Clara Luvanga anayekipiga katika klabu ya wanawake ya Al Nassr nchini Saudia alipachika picha akiwa pamoja na Staa wa timu hiyo, Cristiano Ronaldo iliyoacha maswali mengi kwa mashabiki wake wengine wakidhani imehariria hapa anajibu.
Mapema leo alikuwa mubashara kwenye mtandao wa instagram na kujibu ukweli wa picha hiyo baada ya shabiki mmoja kuuliza kama kweli alipiga na Ronaldo au sanamu lake.
Clara amesema kwa kuwa wanacheza timu moja hakukuwa na ugumu wa kupiga picha kwani aliuomba uongozi wa klabu yake kuwa anaomba picha na staa huyo wa zamani wa Manchester United.
“Nisiwe muongo eti Ronaldo aliniona akaomba picha na mimi hapana. Niliuomba uongozi wa klabu yangu ya wanawake nipate picha na Ronaldo ndio nikapiga naye, basi,” amesema Clara.
Miongoni mwa watu waliompongeza Clara kupiga picha na supastaa huyo ni Rais wa Yanga, Hersi Said na mastaa wenzake aliowahi kucheza nao akiwa Yanga Princess kina Aisha Masaka anayecheza BK Hacken ya Sweden na Maimuna Hamis ‘Mynaco’ anayekipiga Zed FC ya Misri.
Clara ambaye alipita Yanga Princess, Dux Logrono ya Hispania na sasa Saudia, tayari ana medali moja ya ubingwa wa nchi hiyo alikomaliza na mabao 11.