Pokou, Simba freshi asubiri tiketi atue Dar

KIUNGO wa Asec Mimosas Serge Pokou amesema anasubiri tiketi ya ndege kutoka Simba ili atue Dar es Salaam.

Hivi karibuni gazeti hili liliripoti kuwa Simba imefanya mazungumzo na kiungo huyo panga pangua wa Asec na wamekubaliana sehemu kubwa ya dili hilo, ili mwamba huyo aje akakipige kwenye kikosi hicho msimu ujao.

Tayari soko la wachezaji kutoka Asec limeshazoeleka hapa nchini, baada ya mastaa kama Stephane Aziz Ki, Pacome Zouazoua na Aubin Kramo kutoka huko kuja kukiwasha hapa nchini.

Muivory Coast, huyo mwenye mkataba wa mwaka mmoja na Asec, ana historia nzuri na Wekundu wa Msimbazi katika michuano ya kimataifa hatua ya makundi, baada ya kuwavurugia hesabu kwa kuwafunga bao la jioni (dakika 77) katika mchezo wa kwanza msimu huu, walipokutana kwenye Uwanja wa Mkapa uliomalizika kwa sare ya bao 1-1, lakini pia alionyesha kiwango cha juu kwenye mchezo wa pili ugenini.

Akizungumza na Mwanaspoti jana, Pokou mwenye kasi na chenga za maudhi ambaye inaelezwa kuwa ameshaomba kuondoka kwenye timu yake, alisema kila kitu kwake kipo sawa na anachosubiri kwa sasa ni tiketi tu kutoka Simba ili atue Dar es Salaam kwa ajili ya mazungumzo ya mwisho.

 “Nafikiri unakumbuka kuwa awali tulishafanya mazungumzo na Simba, sasa imebaki sehemu ndogo sana,” alisema kiungo huyo mahiri.

“Nilipozungumza nao walianiambia nisubiri kidogo kwani watanipigia simu ili watume tiketi, huku wakisema kuwa mambo wanamalizia. Nafikiri labda ni hadi ligi iishe huko kwenu,” alisema Pokou.

Kinda huyo mwenye miaka 23, ambaye ni panga pangua ya kikosi hicho, amefunga mabao matatu na asisti moja katika Ligi ya Mabingwa Afrika, akifungana na Karamoko kwa rekodi hizo hizo, lakini jamaa ndiye kinara wa mabao kwenye timu yake akiwa na mabao nane kwenye Ligi ya Ivory Coast ikiwa imeshachezwa michezo 28.

Akiwa amewazidi viungo washambuliaji wa Simba ambao ni Clatous Chama na Saido Ntibazonkiza ambao wote ni wakongwe wakiwa na jumla ya mabao saba kila mmoja katika ligi nao wamecheza michezo 27 kabla ya mechi ya jana.

Hivyo anaweza kuwa na nafasi ya kucheza katika kikosi hicho kwani rekodi zinambeba kuliko wachezaji wote walioko Simba msimu huu katika maeneo hayo mawili anayochezea.

Hesabu hizi kama zikienda sawa ina maana Simba inafanya maamuzi ya kumsaka mrithi wa mkongwe Said Ntibazonkiza ‘Saido’ ambaye Mwanaspoti linafahamu kuwa mabosi wa klabu hiyo wana mpango wa kutomuongezea mkataba mwishoni mwa msimu na hivyo nafasi yake itachukuliwa na staa huyo.

Related Posts