Dodoma. Serikali imetoa ufafanuzi kuhusu ukomo wa kuweka alama za upana wa barabara kwa kuzingatia sheria za mwaka 1932 na 2007.
Ufafanuzi huo umetokana na swali la msingi la Mbunge wa Geita Mjini, Constantine Kanyasu ambaye amehoji bungeni leo Mei 21, 2024 akitaka kujua ni upi ukomo wa kuweka alama za upana wa barabara mpaka vijijini na kuwataka wananchi kubomoa nyumba kwa kutumia sheria hizo.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya amesema kwa Sheria ya Barabara ya mwaka 1932, hifadhi ya barabara zinazosimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) zilikuwa mita 22.5 kutoka katikati ya barabara kila upande.
Hata hivyo, amesema kwa barabara ya Morogoro hifadhi ilikuwa kati ya mita 22.5 hadi 121.9 kuanzia Dar es Salaam City Hall hadi daraja la Ruvu.
“Tanroads imeweka alama ya X ya rangi nyekundu kwa mali za wananchi zilizopo ndani ya mita 22.5 na kuwataka waondoe mali hizo kwa gharama zao kwa kuwa wamevamia eneo la hifadhi ya barabara,” amesema.
Amesema Sheria ya Barabara ya Mwaka 2007 iliongeza hifadhi kwa zile zinazosimamiwa na Tanroads kutoka mita 22.5 kuwa mita 30 kutoka katikati ya barabara kila upande.
Amesema katika kutekeleza sheria hiyo, Tanroads imeweka alama ya X ya rangi ya kijani kuonyesha eneo la mita 7.5 liliongezeka kila upande hivyo wananchi waliopo eneo hilo hawapaswi kuondoa mali zao mpaka watakapolipwa fidia.
Katika swali la nyongeza, mbunge wa Kibamba, Issa Mtemvu ametaka viongozi wa wilaya na mkoa kutoa majibu rasmi kwa wakazi walioondolewa kupisha upanuzi wa barabara kwa njia nane kutoka Kimara jijini Dar es Salaam hadi Kibaha mkoani Pwani akisema Sheria ya Mwaka 1932 ndiyo iliyotumika katika upanuzi huo.
“Wananchi wanaendelea na sintofahamu kuhusu kuvunjiwa, je, Serikali ipo tayari kutoa maelekezo kwa mamlaka za mikoa na wilaya kutoa majibu rasmi kwa wananchi ili wasiendelee kuja katika ofisi za mbunge?” amehoji.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Kasekenya, amesema barabara ya Dar es Salaam hadi Ruvu kulikuwa na maeneo ambayo hifadhi ya barabara ni mita 22.5 na mengine hadi mita 121.
Amesema watu wa Kibaha wanapaswa kujua kuwa sheria iliyotumika ni ya mwaka 1932.