Unguja. Wizara ya Afya Zanzibar, imeingia mkataba na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef) wa ununuzi wa vifaa kwa ajili kuboresha huduma za afya hususani mama na mtoto kisiwani hapa.
Kupitia mkataba huo wa manunuzi wenye thamani ya Dola za Marekani 12.5 milioni (Sh32.3 bilioni), Unicef itasaidia utoaji wa dawa muhimu na bidhaa za lishe, vifaa vya matibabu kwa ajili ya vituo vya afya vilivyofanyiwa ukarabati, magari kwa ajili ya idara ya huduma za kinga na timu ya uratibu wa miradi.
Kazi nyingine itakayofanywa ni kutoa vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) na mtandao kwa vitengo 142 vya afya ya msingi (PHCU+).
Akizungumza wakati wa kusaini makubaliano hayo leo Jumanne, Mei 21, 2024 Waziri wa Afya, Ahmed Mazrui amesema ushirikiano huo ni hatua kubwa kuelekea kuendeleza mfumo wa huduma ya afya kupitia Mpango wa Uwekezaji wa Afya ya Mama na Mtoto Tanzania (TMCHIP).
Mpango huo unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, ulianza mwaka 2023 hadi 2027 kwa Dola za Marekani 25 milioni (Sh64.7 bilioni).
“Mpango huu sio tu mpango bali ni safari ya mageuzi inayolenga kuunda mfumo thabiti wa utoaji wa huduma za afya ambao unamhudumia kila mtu, hasa makundi yaliyo hatarini zaidi ambayo ni kinamama, watoto na vijana.
“Tumedhamiria kuinua viwango vya matunzo katika kila ngazi, kuhakikisha kwamba kila mama na mtoto wanapata huduma bora zaidi za afya,” amesema
Kadhalika wataimarisha na kuboresha upatikanaji na utumiaji wa mifumo ya kielektroniki katika huduma ya afya.
“Tunalenga kufanya huduma za afya ya uzazi ziwe rahisi zaidi hasa kwa vijana, katika vituo vya afya na ndani ya jamii,” amesema Mazrui.
Naye mwakilishi wa Unicef nchini Tanzania, Elke Wisch amesema ushirikiano huo ulioanzishwa kati ya Amesema Serikali, Unicef na WB, unaashiria dhamira ya washirika wote katika kuweka vipaumbele vya ustawi wa wanawake na watoto na kuweka msingi mzuri wa afya ya Zanzibar.
Amesema Unicef ina uzoefu wa miaka kadhaa katika eneo hili na iko katika nafasi ya kipekee ya kuchota utaalamu na mbinu bora duniani kote, ili kuifanya Zanzibar kuwa mfano wa ubora katika afya ya kidijitali.
Miongoni mwa mafanikio muhimu ya ushirikiano wa afya ya kidijitali kati ya Serikali ya Zanzibar na Unicef ni kubuni na kuendeleza maoni ya wateja, ijulikanayo kama (Zan Afya Maoni), na kubuni na kutengeneza zana ya kidijitali inayounga mkono usimamizi wa wafanyakazi wa afya.
“Kupitia mkataba huu, Unicef ina furaha kuchangia katika kuboresha utoaji wa huduma kupitia ununuzi wa vifaa vya matibabu vya ubora wa juu na bidhaa nyingine za afya, ikiwa ni pamoja na maabara, na vifaa vya ICT,” amesema Wisch.