Simba yaendelea kukimbiza Azam | Mwanaspoti

Simba imeendelea kuifukuza Azam FC baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-1, dhidi ya Geita Gold kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Uwanja wa Azam Complex.

Ushindi huo umeifanya Simba kufikisha pointi 63 sawa na Azam ambayo imebaki juu nafasi ya pili kwa faida ya tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa ambapo mapema imeshinda ugenini kwa mabao 2-0 dhidi ya JKT Tanzania.

Simba imelazimika kutoka nyuma kutengeneza ushindi huo baada ya Geita kutangulia kupata bao dakika ya 11 mfungaji akiwa kiungo Geofrey Julius aliyemalizia kirahisi baada ya mpira uliomshinda kipa wa wekundu hao Hussein Abel.

Hata hivyo, Simba ikasawazisha bao hilo dakika za mwisho za kipindi cha kwanza kwa mkwaju wa penalti mfungaji akiwa Said Ntibazonkiza ‘Saido’ baada ya beki wake Shomari Kapombe kuangushwa eneo la hatari timu hizo zikienda mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.

Kipindi cha pili kuingia kwa kiungo Willy Onana dakika ya 65 kuliibadilisha Simba na kuongeza kasi ya mashambulizi kwenye lango la Geita.

Geita ikapata pigo dakika ya 68 baada ya nahodha wake Samwel Onditi kupewa kadi ya pili ya njano iliyozaa nyekundu, baada ya kumuangusha Onana na mwamuzi Omari Mdoe kutoka Tanga kumtoa nje.

Simba ilitumia nafasi hiyo kupata bao la pili, dakika ya 72, mfungaji akiwa Saido tena,  akifunga bao lake la tisa msimu huu  kiufundi kwa  mpira wa adhabu ndogo iliyotokana na Onana kuangushwa.

Onana aliendelea kuirudisha Simba mchezoni akitengeneza bao la tatu kwa timu akitoa asisti kwa Ladack Chasambi dakika ya 86.
Chasambi akakamilisha ushindi wa Simba akifunga bao la nne na la pili kwake dakika ya 90+3 kwa shuti Kali la mguu wa kushoto akigongeana vizuri na Mzamiru Yassin na kuifanya mchezo huo kumalizika kwa Wekundu hao kushinda kwa mabao 4-1.

Related Posts