Tabora, Ihefu mechi ya matumaini

LEO Jumatano katika Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Tabora kutapigwa mechi ya kibabe kati ya wenyeji Tabora United na Ihefu ambayo imebeba matumaini makubwa ya timu hizo mbili kwa msimu huu.

Mchezo huo ni wa Ligi Kuu Bara mzunguko wa 28 kwa kila timu na matokeo yoyote yatakayopatikana yatabadili mambo mengi hususan kwenye nafasi ambazo timu hizo zipo kwenye msimamo kwani Ihefu ni ya saba na alama 32, huku Tabora ikiwa ya 14 na pointi 26.

Ihefu bado ina matumaini ya kumaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo huku Tabora ikipambana kujinasua kwenye mtego wa kushuka daraja ambapo kila timu imebakiza mechi tatu pekee katika ligi.

Ihefu ambayo Jumapili ilicheza nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), dhidi ya Yanga na kufungwa bao 1-0, inawania kumaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo lakini inakabiliwa na ushindani wa timu za Coastal Union, KMC na Tanzania Prisons ambazo zipo juu yake kwenye msimamo Sambamba na mabingwa Yanga, pia Azam na Simba zilizojihakikishia kumaliza katika nafasi tatu za juu. Mechi mbili za mwisho za Ihefu itakutana na Dodoma Jiji pia Mtibwa Sugar.

Kwa upande wa Tabora, inahitaji ushindi kwenye mechi hiyo ili kurejesha matumaini ya kusalia kwenye ligi kwa msimu ujao kwa kuwa baada ya hapo itakuwa imebakiza mechi mbili ngumu ugenini dhidi ya Mabingwa Yanga kisha Namungo inayoshika nafasi ya nane kwenye msimamo.

Kwa hesabu za haraka kama mchezo huo utamalizika kwa sare utakuwa umetibua hesabu za timu zote mbili  hali kadharika kwa timu itakayopoteza mchezo itapata pigo zaidi.

Moja ya vitu vinavyoongeza mvuto na ushindani wa mechi hiyo ni ubora wa wachezaji wa kigeni kwenye kila kikosi ambapo kati ya 11 wanaoanza katika kila timu, sita hadi saba wanatokea mataifa mengine huku wazawa wanaopata nafasi wakiwa wachache.

Pamoja na hivyo, Ihefu inarekodi tamu mbele ya Tabora kwani katika mechi ya mwisho timu hizo mbili zilipokutana Wauaji wa Kusini hao walishinda kwa mabao 2-1 mbele ya Wanatabora hao.

Rekodi nyingine, Ihefu ina matokeo bora katika mechi tano za ligi zilizopita ilizocheza ukilinganisha na Tabora iliyopanda Ligi Kuu msimu huu, kwani wakali hao kutoka Ruangwa wameshinda tatu, sare moja na kupoteza moja huku wenyeji wakiwa wameshinda mchezo mmoja pekee, kuchapwa mitatu na suluhu moja.

Marouf Tchakei ndiye mchezaji mwenye takwimu bora zaidi kwa Ihefu akiwa amefunga mabao tisa kwenye ligi akifuatiwa na Elvis Rupia mwenye matano, huku kwa Tabora kinara akiwa Eric Okutu aliyefunga mara saba akifuatiwa na Ben Nakibinge aliyecheka na nyavu mara nne na huenda mechi hiyo ikawa na mabao mengi kutokana na uhitaji wa kila timu.

Kaimu kocha mkuu wa Tabora United, Masoud Djuma ameweka wazi uhitaji wa mechi hiyo akisema amekiandaa kikosi chake kupata ushindi.

“Mechi za mwisho zinakuwa ngumu. Kila timu inatafuta ushindi ili imalize katika eneo zuri lakini kwetu sisi tunauhitaji zaidi na ili tufikie malengo, ni lazima tushinde mechi zilizobaki ikiwemo hii dhidi ya Ihefu,” amesema Juma raia wa Burundi aliyewahi kuzinoa Simba na Dodoma Jiji za Ligi Kuu.

Mkuu wa benchi la ufundi la Ihefu, Mecky Maxime amesema wachezaji wake wana uchovu baada ya mechi ya FA dhidi ya Yanga lakini hawana budi kupambana kuhakikisha wanashinda dhidi ya Tabora.

“Ratiba ni ngumu na kwa bahati mbaya zaidi ni mechi muhimu ambazo hatupaswi kuzubaa. Tunaandaa timu kukabiliana na hali. Tunataka kushinda na tunaamini tutafanya hivyo licha ya kuwa na uchovu kwa baadhi ya wachezaji,” amesema Maxime aliyewahi kuzinoa Mtibwa Sugar na Kagera Sugar za Ligi Kuu.

Ikumbukwe msimu huu timu nne zitakazomaliza katika nafasi za juu zitashiriki michuano ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa ngazi ya klabu lakini mbili za mwisho zitashuka daraja moja kwa moja na zitakazomaliza zikiwa namba 14 na 13 zitacheza mechi za mtoano (play off) kuwania kusalia kwenye ligi hiyo.

Related Posts