Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) liko mbioni kubatilisha uamuzi wa fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) kuchezwa katika Uwanja wa Tanzanite uliopo Babati, Manyara mapema mwezi ujao huku viwanja vitatu vikitajwa kupewa nafasi kubwa kuchukua fursa hiyo.
Viwanja vitatu vinavyopewa nafasi kubwa kuchukua fursa ambayo Uwanja wa Tanzanite, Babati inaelekea kuikosa ni Benjamin Mkapa (Dar es Salaam), Sheikh Amri Abeid (Arusha) pamoja na CCM Kirumba (Mwanza).
Kamati ya Utendaji ya TFF inatarajiwa kukutana wiki hii jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya uamuzi wa mwisho wa kuchagua uwanja ambao utaandaa mechi hiyo ya fainali ambayo itazikutanisha Yanga na Azam.
Habari kutoka kwa chanzo cha uhakika ndani ya TFF zimelithibitishia gazeti hili kuwa kutokana na sababu mbili ambazo zimeonekana zina mashiko, mechi hiyo ya fainali haitachezwa Babati kama ambavyo ilipangwa awali.
“Kamati ya utendaji inakutana wiki hii kuamua uwanja ambao utaanda fainali ya Kombe la Shirikisho la FA na tayari ina majina ya viwanja ambavyo vinaweza kuchukua nafasi hiyo kwa haraka kutokana na kutohitaji marekebisho makubwa.
“Uwanja wa Babati ule ni mzuri kwenye nyasi lakini una kasoro kadhaa ambazo sio rahisi kuweza kuzirekebisha ndani ya muda mfupi kabla ya fainali,” kilisema chanzo hicho.
Uchache wa idadi ya mashabiki ambao uwanja huo unaweza kuingiza umetajwa kama sababu moja iliyochangia TFF kuchukua uamuzi huo lakini nyingine ni uhaba wa huduma ya malazi kwa umati wa mashabiki ambao watakwenda kutazama mchezo huo.
Uwanja huo wa Tanzanite una jukwaa moja dogo ambalo limetengwa maalumu kwa ajili ya watu wa VIP, hivyo idadi kubwa ya mashabiki ambao wataenda kutazama mechi hiyo watalazimika kusimama lakini inakadiriwa kuwa unaweza kuingiza idadi ndogo ya mashabiki wasiozidi 10,000.
Kana kwamba haitoshi uchache wa hoteli na nyumba za kulala wageni ni sababu nyingine ambayo inatajwa kushawishi vigogo wa TFF kuamua kuhamisha kituo cha mchezo huo wa fainali kutoka Babati kwenda kwingine ili kuepusha usumbufu kwa wageni na mashabiki ambao wamepanga kutazama mechi hiyo lakini pia kutokamilika kwa baadhi ya vitu ambavyo vilitakiwa.
Gazeti hili linafahamu kuwa mchezo wa nusu fainali baina ya Yanga na Ihefu uliofanyika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha juzi, umechangia kwa kiasi kikubwa shirikisho kufanya uamuzi wa haraka.
Katika mchezo huo ambao Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0, umati mkubwa wa mashabiki ulishindwa kuingia ndani ya uwanja huo kwa ajili ya kutazama mechi hiyo licha ya wengi wao kuwa na tiketi halali.
Hilo lilichangia kuibuka kwa vurugu za hapa na palepale zilizotokana na mashabiki hao kulazimisha kuingia ndani ya uwanja huku baadhi wakilazimika kuingia kwa kuruka ukuta jambo lililohatarisha usalama wao.
Juhudi za kumtafuta mkurugenzi wa habari na masoko wa TFF, Boniface Wambura kuzungumzia suala hilo ziligonga mwamba kutokana na simu yake kuita bila kupokelewa kama ilivyokuwa kwa mkurugenzi wa mashindano, Salum Madadi.
Baada ya wote kukosekana, Msemaji Msaidizi wa TFF Inocent Okama, alisema maamuzi yote yatatolewa na TFF na hadi sasa hakuna mabadiliko aliyopewa.
Uamuzi wa mechi ya fainali kuchezwa kwenye Uwanja wa Tanzanite ulitangazwa na Rais wa TFF, Wallace Karia, Aprili 2 wakati wa kusaini makubaliano ya mkataba wa udhamini wa mashindano hayo.
“Tunapeleka mashindano haya Manyara kutoa shukrani na sapoti kwa juhudi ambazo zinafanywa na maeneo husika na kuendeleza mpira huko. Kuna baadhi ya mikoa tumeipa changamoto hiyo, warekebishe miundombinu ili tuweze kuwapa nafasi hiyo.”
Viwanja vitatu ambavyo vinapewa nafasi ya kimojawapo kuandaa mechi ya fainali badala ya ule wa Tanzanite, Babati, vyote vimewahi kuandaa fainali ya mashindano hayo kwa nyakati tofauti.
Uwanja wa Benjamin Mkapa uliandaa fainali ya msimu wa 2015/2016 ambayo Yanga iliibuka na ushindi baada ya kuifunga Azam FC kwa mabao 3-1 wakati Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza uliandaa fainali ya msimu wa 2017/2018 ambayo Mtibwa Sugar iliibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Singida United.
Fainali kwenye Uwanja wa Sheikh Amri ilichezwa msimu wa 2021/2022 ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa mikwaju ya penalti 4-1 dhidi ya Coastal baada ya timu hizo kutoka sare ya mabao 3-3 katika dakika 120 za mchezo.