VIDEO: Sababu kufanyika ibada ya wafu makaburi ya Igoma Mei 21 kila mwaka

Mwanza. “Ilikuwa siku ya masikitiko, mji ulikuwa ukiwa, tuliokuwa shuleni hatukuendelea na mitihani.” 

Ni kauli ya Paroko wa Kanisa Katoliki Parokia ya Nyamhongolo Jimbo Kuu la Mwanza, George Nzungu akisimulia namna tukio la ajali ya MV Bukoba lilivyokuwa.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Mei 21, 2024 katika eneo la Igoma Jijini Mwanza yalipo makaburi ya watu waliofariki dunia kutokana na ajali ya Meli ya Mv Bukoba, Padri Nzungu amesema kamwe hatoisahau siku hiyo, ndiyo maana hufanya Ibada maalumu ya wafu makaburini hapo kila ifikapo Mei 21, kama kumbukumbu ya kuwaenzi marehemu hao na kuzidi kuwaombea walionusurika na ajali.

Meli ya MV Bukoba ilipata ajali Mei 21, 1996 kilomita zisizozidi mbili kutoka eneo la Bwiru wilayani Ilemela mkoani Mwanza, meli hiyo ilikuwa ikitokea Bukoba mkoani Kagera.

Na leo Jumanne ndiyo kumbukizi ya miaka 28 tangu kutokea kwa ajali hiyo iliyosababisha vifo vya watu zaidi ya 900 na wengine kunusurika.

Hata hivyo, Mwananchi lililofika eneo hilo la makaburi limeshuhudia idadi ndogo ya ndugu waliofika kufanya ibada maalumu ya kuwaombea ndugu zao waliopumzishwa kwenye makaburi hayo.

Awali, Serikali na taasisi za dini zote mkoani humo zilikuwa zikiendesha ibada maalum ya maombezi kwa ajili ya kumbukizi ya ajali hiyo ambayo makovu yake bado hayajafutika miongoni mwa waliopoteza wapendwa wao.

Kwa mujibu wa Padri Nzungu, kuna ulazima wa kurejesha utaratibu wa kumbukizi hiyo kwa kuendesha ibada maalumu ya maombi katika eneo la makaburi ili kuwaenzi waliofariki dunia katika ajali hiyo.


Sababu kufanyika ibada makaburi ya Igoma Mei 21 kila mwaka

“Hili tukio ni la kihistoria, nakumbuka siku hiyo (Mei 21, 1996) tulikuwa tunafanya mitihani ya kidato cha nne pale Mwanza Sekondari. Ghafla tulianza kuona misururu ya magari ikipandisha Bugando, ilikuwa siku ya masikitiko, Mji ulikuwa ukiwa na tuliokuwa shuleni hatukuendelea na mitihani,” amesema Padri Nzungu.

Amesema siku ya ajali, alishuhudia miili zaidi ya 300 ikiwa imelazwa sakafuni ndani ya chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Bugando (Kwa sasa ni ya Rufaa ya Kanda ya Bugando) jijini humo huku miili mingine ikiendelea kuopolewa ziwani na kupelekwa hospitalini hapo.

Amesema kwake siku hiyo haitosahaulika maishani mwake, na hiyo ndiyo inampa msukumo wa kufanya ibada maalumu makaburini hapo kila ifikapo Mei 21 ya kila mwaka.

Hata hivyo, amesema hapendezwi na hali ilivyo hivi sasa ya watu wachache kujitokeza kuadhimisha siku hiyo kwenye ibada ya wafu inayofanyika eneo hilo tofauti na miaka ya nyuma ambapo  lilijaa watu wakiwa na mashada ya maua kwa ajili ya kuyaweka kwenye makaburi ya wafu hao baada ya Ibada.

“Serikali na jamii inapaswa kutumia siku ya kumbukizi ya tukio hili la ajali ya MV Bukoba kutafakari namna bora ya kuwaenzi waathiriwa, kuboresha mifumo ya usafirishaji majini na kuangalia tunapolega ili tukio la aina hii lisijirudie tena,” amesema Padri Nzungu.

Simulizi ya Padri Nzungu inaungwa mkono na Mkazi wa Bukoba vijijini mkoani Kagera, Juma Lutaiwa aliyesafiri kuja Igoma yaliko makaburi kwa kushiriki Ibada hiyo maalumu ya kumbukizi ya wafu hao.

Lutaiwa amesema katika ajali hiyo alimpoteza dada yake aliyekuwa akiitwa Rosemary Ijumba.

Amesema hatosahau namna alivyoagana na dada yake aliyekuwa akisafiri kwenda jijini Mwanza kwa ahadi angerejea lakini alifia majini.

“Ninamkumbuka sana dada yangu Rosemary, bado hatujamsahau, tutaendelea kuwa tunakuja hapa Igoma kufanya ibada kwa ajili yake. Japo naona mwitikio wa watu unazidi kupungua tofauti na miaka ya nyuma,” amesema Juma.

Ametoa wito kwa Watanzania na Serikali, kuendeleza maadhimisho ya siku hiyo kama awali na wasiiche ikajifia.

Baadhi ya ndugu waliopoteza wapendwa wao katika ajali ya MV Bukoba wakifanya ibada katika makaburi walipozikwa baadhi ya waliokufa katika ajali hiyo. Picha na Mgongo Kaitira

Mkazi wa Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza, Jimmy Luhende amesema anashangaa kuona kila mwaka idadi ya watu wanaofika makaburini hapo kwa ajili ya kufanya ibada inazidi kupungua tofauti na awali kulikuwa na umati mkubwa.

Akitolea mfano wa mauaji ya kimbali nchini Rwanda, Luhende amesema kila mgeni anayetembelea Jiji la Kigali, hushauriwa kutembelea eneo yalikofanyika mauaji ya kimbari.

Amesema lengo la nchi hiyo ni kutaka kutoa elimu na historia ya mauaji hayo kwa kila mtu anayefika nchini humo.

Amesema hata Tanzania pia inapaswa kufanya hivyo badala ya kuacha historia ya ajali hiyo ya MV Bukoba ikapotea.

Hivyo, ameiomba Serikali pia kutafuta watalaamu watakaozamia eneo ilipozama na kunasua meli hiyo ili mabaki yake yaopolewe na kuwekwa eneo la Igoma yalipo makaburi hayo ili kulifanya eneo hilo kuwa la kihistoria zaidi.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli nchini (Tasac) Mohamed Salum amesema wakati nchi inafanya kumbukizi ya ajali hiyo, wakala huo unaendelea kuchukua hatua ili kuhakikisha hakuna mtu anayefariki kwa ajali ya majini nchini.

“Serikali inachukua hatua kuhakikisha vitu na vyombo vinavyotembea majini vinakuwa salama, tunajenga kituo kikuu cha utafutaji na uokozi eneo la Uwanja wa Ndege mkoani Mwanza na tutahakikisha kuna mfumo na vyombo vya uokozi majini wakati wote,” amesema Salum.

Amesema mbali na kituo hicho, Tasac imeanza mchakato wa kujenga vituo vingine vya utafutaji na uokozi Musoma (Mara), Sengerema (Mara) na mkoani Kagera ili kuboresha huduma ya usafirishaji kwa njia ya maji nchini.

“Pia tunahakikisha vyombo vinavyojengwa vinafuata kanuni za ujenzi kama ni michoro tunahakikisha inaletwa kukaguliwa ili iendane na chombo kilichokusudiwa. Pia tunaimarisha elimu za mabaharia,” amesema.

Mbali na Mv Bukoba, matukio mengine yanayohusisha vyombo vya majini ni pamoja na ajali ya Kivuko cha Mv Nyerere iliyotokea Septemba 20, 2018 na kusababisha watu zaidi ya 220 kupoteza maisha,  kivuko hicho kilikuwa kinafanya safari zake kati ya Ukerewe na kisiwa cha Ukara mkoani Mwanza.

Ajali nyingine ilitokea Septemba 10,2011, ikihusisha Meli ya Mv Spice Islander iliyozama kwenye mkondo wa Nungwi ikitokea Unguja kuelekea Pemba, zaidi ya watu 1,000 waliripotiwa kufa, huku mali isiyojulikana thamani yake ikizama pia.

Related Posts