Bukombe. Vyama vya ushirika 334 kati ya 590 vilivyopo mkoani Geita vimefilisika na kushindwa kujiendesha kutokana na kukosa mitaji toshelevu
Kufilisika kwa vyama hivyo kumetokana na mabadiliko ya sheria ndogo za huduma ndogo za fedha zinazotaka chama kiwe na mtaji usiopungua Sh10 milioni pamoja na kuwa kwenye mfumo wa ‘move’, jambo lililofanya vyama vingi kukosa sifa.
Akizungumza kwenye Jukwaa la Ushirika lililofanyika wilayani Bukombe, Mrajisi wa Ushirika mkoani humo, Doreen Mwanri amesema vyama hai ni 256 kutokana na wanachama kutofanya shughuli zao kama walivyojisajili.
“Ili chama kiweze kusajiliwa kwenye mfumo wa ‘move’ au kutambulika kwenye sheria ndogo, kinapaswa kuwa na mtaji wa Sh10 milioni na kwa kuwa vingi havifanyi kazi, havina mtaji na wanachama wengi bado hawajakubaliana na mabadiliko ya sheria, tunaendelea kuwaelimisha,” amesema Mwanri.
Amesema sababu nyingine ni kuhamahama kwa wavuvi ambao ni moja ya shughuli kubwa zinazofanywa kwenye mkoa huo.
“Wavuvi wengi wanaanzisha vyama vya ushirika lakini wanahamahama au wakiona changamoto ya kupatikana kwa samaki, wanaacha wanaenda kwenye shughuli nyingine na kuacha chama hakijiendeshi,” amesema.
Mrajisi huyo amesema kutokana na shughuli za madini kuwa moja ya fursa za kiuchumi kwenye mkoa huo wachimbaji wengi hujiunga kwenye vyama vya ushirika, lakini kutokana na kutoamiana, hushindwa kufanya kazi kwa umoja na kusababisha chama kufa.
“Kutokana na changamoto hizo, tumeendelea kutoa elimu pamoja na kushauri waungane lakini kuna changamoto wengine hawataki kuungana kutokana na mtazamo,” amesema.
Baadhi ya wanaushirika wakizungumza kwenye kongamano hilo, wamesema mabadiliko ya sheria ndogo za fedha za mwaka 2019, imewafanya wanachama wakate tamaa na kushindwa kuendelea na ushirika.
“Sheria hiyo ndogo iliamuru vikundi vyote vyenye mtaji wa Sh10 milioni visajiliwe kama saccos, imeingiliana na vyama vilivyokuwa na mipango yao, wanakusanya fedha na mwisho wa mwaka wanagawana. Lakini katika mabadiliko ya sheria Serikali ndio inapanga matumizi, hii imefanya watu wapate wasiwasi na itaendelea kuua ushirika,” amesema mwanaushirika, Martin Shija.
“Lengo la mwanaushirika ni kupata faida kwenye kile walichozalisha lakini sasa Serikali inabana msitumie, imewapa watu wasiwasi na hii itasababisha vyama kuendelea kufa,” amesema Shija.
Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Paskasi Muragili amesema pamoja na sekta ya madini kuingizwa kwenye vyama vya ushirika, ipo changamoto ya uelewa wa maana ya ushirika, hivyo kusababisha wanaonufaika kuwa wachache.
“Kwenye sekta ya madini bado inahitajika elimu ya kutosha, ipo migogoro mingi wanaingia kwenye mikataba na wawekezaji lakini wanaponufaika ni viongozi, lakini wanachama wengine hawapati manufaa kabisa na ndio maana tunaendelea kuwapa miongozo ili wote wanufaike,” amesema
Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Mohamed Gombati amevitaka vyama vya ushirika mkoani humo kujikita kwenye fursa za ufugaji na uvuvi kwa kuwa ni eneo lisilochangamkiwa kama kwenye kilimo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela amesema changamoto kubwa kwenye vyama vya ushirika ni baadhi ya wanachama kukosa elimu ya ushirika.