Wabunge wataja kinachokwamisha biashara | Mwananchi

Dodoma. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuingilia akaunti za wafanyabiashara benki, wawekezaji kutolipa mafao ya wafanyakazi, ugumu wa wazawa kufungua biashara na suala la ‘rumbesa’ ni miongoni mwa kero zilizoelezwa na wabunge kuwa zinakwamisha biashara nchini.

Wabunge walieleza vikwazo hivyo, wakati wakichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara iliyowasilishwa bungeni Mei 21, 2024.

Akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi hayo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji aliliomba Bunge kuidhinisha Sh110.8 bilioni kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Kati ya fedha hizo, Sh81.1 bilioni ni matumizi ya kawaida na Sh29.9 bilioni ni matumizi ya maendeleo.

Akichangia mjadala huo mbunge wa Vunjo, Dk Charles Kimei amesema TRA imekiuka agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la ukomo wa miaka mitatu, ya kufanya tathmini ya hesabu zinazodaiwa kwa kampuni za kibiashara.

Dk Kimei, licha ya kumpongeza Waziri Kijaji kwa kufanya mazungumzo na wafanyabiashara ili kutatua changamoto zinazowakabili, amemtaka azungumze na wafanyabiashara wazawa wanaolalamikia ugumu wa kuanzisha au kufanya biashara nchini.

Amesema bado wapo wawekezaji wazawa wanapata changamoto ya kutakiwa kukaguliwa na TRA hesabu za miaka ya nyuma, licha ya kuwa Rais Samia aliweka ukomo.

“Wanalalamika kwa mfano, Rais Samia aliweka ukomo wa TRA kukagua au kutathmini hesabu za kampuni ili kuona kama zililipa kodi zao sawasawa, lakini bado wanaenda wanataka hesabu za miaka mitatu kwa kisingizio cha tathmini… ule ukomo haufanyi kazi, halafu ule ukomo haujawekwa katika waraka ambao ungeweza kutekelezeka na TRA,” amesema.

Dk Kimei alimwomba Waziri Kijaji aangalie namna anavyoweza kufanya kwa maagizo ambayo yametolewa na mamlaka yaweze kutekelezeka ili wafanyabiashara na wawekezaji wafanye shughuli zao kwa amani na utulivu.

Amesema tatizo lingine ni TRA kukagua akaunti za watu na kampuni kwenye benki na kuagiza mtu ambaye hajalipa kodi fedha zake zitolewe kwenye akaunti pindi atakapokuwa amepata malipo yoyote.

Dk Kimei pia alizungumzia kero 300 za biashara zinazoelezwa zimeondolewa, akisema zinapaswa kuwekwa wazi, ili wafanyabiashara wazione, badala ya kutolewa maelezo pekee.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Kilumbe Ng’enda amesema wizara hiyo bado ina kazi kubwa ya kulisaidia Taifa na kuhakikisha inajenga uwezo kwa wananchi wa kusisimua ufanyaji biashara badala ya kubaki wapagazi au wafanyakazi wa wafanyabiashara.

“Jambo pekee linaloweza kutusaidia kutuongezea nguvu ni biashara, na kwa nini nasema biashara kwa sababu inayo vigezo. Ukishakuwa na bandari, barabara na reli halafu majirani zako wana mahitaji ya vitu vinapita kwako unaweza kufanya biashara vizuri,” amesema.

Kilumbe amesema mpaka sasa takwimu zilizotolewa na Baraza la Biashara la Afrika Mashariki zinaonyesha katika mwaka wa 2019 hadi 2021, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambayo asilimia 80 hadi 85 ya mahitaji yake yanatoka nje ya nchi hiyo, Tanzania ipo nafasi ya saba katika kuingiza mizigo nchini humo.

Amesema China ndilo Taifa la kwanza linalofanya biashara na DRC, likifuatiwa na Afrika Kusini, Zambia, Kenya, Rwanda na Tanzania ikiwa ya saba, licha ya kupakana nayo.

“Hatujawa makini, tumeshindwa kufanya biashara pamoja na bandari tuliyonayo na miundombinu na ujirani tulionao. Tunaposema wizara hii (Viwanda na Biashara) mmekabidhiwa kazi ya kuleta msisimko wa kibiashara ili uchangie katika pato la Taifa, lazima mwende mbele kujiongeza na kuangalia fursa zilizopo,” amesema.

Mbunge wa Viti Maalumu, Sophia Mwakagenda amesema kuna tatizo kwa wawekezaji kutowalipa mafao wafanyakazi, malipo madogo na saa za kazi ni nyingi kuliko wanacholipwa.

Amesema mwekezaji anapoamua kufunga kiwanda isiwe ghafla, lazima taarifa zitolewe mapema ili stahiki za wafanyakazi zijulikane na wakulima waliolima mazao kwa ajili ya kiwanda hicho nao waelezwe mapema kuliko kuachwa wasijue wauze wapi mazao yao.

Mwakagenda ametaka mifumo ya Serikali isomane kwa kuwa kufungwa kwa kiwanda cha chai Rungwe, Wizara za Kilimo pamoja na Viwanda na Biashara zilipaswa kufahamu namna wafanyakazi watakavyopata stahiki zao na wakulima watapeleka wapi mazao yao.

Mbunge huyo amesema wafanyakazi wanafanyishwa kazi kuanzia saa moja asubuhi hadi saa 12 jioni na wanapewa ujira wa Sh5,000.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, imezungumzia upimaji wa mazao ya wakulima kwa kujaza magunia bila kufuata vipimo rasmi, ‘rumbesa’, ikisema siyo sahihi.

Mjumbe wa kamati hiyo, Francis Mtinga, akiwasilisha maoni ya kamati kwa niaba ya Mwenyekiti, Deodatus Mwanyika, amesema:

“Wapo baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu ambao wameendelea kutumia mfumo wa rumbesa kuuza/kununua bidhaa, hasa mazao ya wakulima, kwa lengo la kuwanyonya na kuikosesha Serikali mapato”.

Ametoa ushauri wa kamati kuhusu rumbesa akisema Serikali iendelee kutoa elimu kwa wananchi sehemu mbalimbali kuhusu faida ya kuuza kwa kutumia vipimo sahihi (mizani) na athari inayopatikana kwa kutumia rumbesa.

“Serikali itoe mwongozo kuhusiana na suala la rumbesa ambalo ni mtambuka, ili halmashauri zote ziweze kusimamia kwa uwiano ambao utaleta manufaa kwa wakulima,” amesema.

“Wakurugenzi wa halmashauri na watendaji wengine wanaohusika, wahakikishe wakulima hawadhulumiwi wanapouza mazao yao,” amesema.

Kwenye hotuba yake, Waziri Kijaji alisema wizara kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ina vipaumbele sita vitakavyotekelezwa.

Amevitaja vipaumbele hivyo ni kuendelea na utekelezaji wa miradi ya kielelezo na kimkakati, kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma kwa kuimarisha miundombinu na mazingira wezeshi na kuboresha mazingira ya biashara.

Pia, ametaja kuchochea maendeleo ya watu kwa kuboresha miradi na programu katika sekta ya jamii inayohusisha elimu na mafunzo ya ujuzi, kuendelea na utafutaji wa masoko kwa bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini pamoja na kuchochea ukuaji wa sekta binafsi nchini.

Dk Kijaji amesema shughuli zitakazotekelezwa kwa kuzingatia vipaumbele vikuu vya wizara ni kuanzisha mitaa ya viwanda kwa ajili ya kongano za viwanda na biashara katika wilaya moja kila mkoa, ili kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Pia, kuendelea kupambana na uingizaji wa bidhaa bandia ili kulinda nembo au alama za bidhaa dhidi ya watu wanaotumia nembo/alama hizo bila idhini ya wamiliki, kuendeleza miradi ya kimkakati ya magadi soda Engaruka, makaa ya mawe Mchuchuma na Chuma Liganga.

Shughuli nyingine zitakazofanyika ni kusanifu na kuendeleza utengenezaji wa vifaatiba vya hospitali awamu ya tatu, utengenezaji wa kibiashara wa viwanda vidogo vya kuchakata sukari na kutengeneza mitambo ya nishati mbadala na teknolojia za wachimbaji wadogo wa madini (ASM) ili ziweze kusaidia katika utunzaji wa mazingira.

Dk Kijaji akizungumzia fidia amesema wizara chini ya uratibu wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) imeendelea na ukamilishaji wa ulipaji wa fidia kwa wananchi wanaopisha mradi unganishi wa Mchuchuma na Linganga.

“Hadi kufikia Machi, 2024, jumla ya Sh15.414 bilioni zimelipwa kati ya Sh15.424 bilioni kwa wafidiwa 1,129 kati ya 1,142. Idadi ya wafidiwa waliolipwa ni sawa na asilimia 99. Kiasi ambacho hakijalipwa kwa wafidiwa 13 ni Sh10.227 milioni,” amesema.

Amesema wananchi hao 13 ambao hawajalipwa ni kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo baadhi yao kutojitokeza, na wengine kutokukamilika kwa nyaraka na taratibu za mirathi.

Related Posts