Wanafunzi wanaosomeshwa na Ngorongoro walia kusalitiwa, wajibiwa

Dar es Salaam. Kuwacheleweshe fedha ya karo na za kujikimu kwa wanafunzi 554 wa Sekondari na vyuo kumeibua mvutano mpya kati ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Baraza la Wafugaji Tarafa ya Ngorongoro (NPC).

Msingi wa mvutano huo ni kitendo cha (NCAA), kushindwa kutekeleza matakwa ya mkataba walioingia tangu mwaka 1994 wa kusomesha wanafunzi hao wanatoka mazingira magumu bila kutoa taarifa, huku NPC ikidai huo ni usaliti mkubwa wanaofanyiwa.

Ukinzani huo unajengwa na hoja kuwa wakati NPC wanaingia mkataba na NCAA, walikubaliana watakuwa wanatoa gharama za kusomesha wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza, cha tano, vyuo vya kati na vyuo vikuu na kuwapa fedha za kujikimu.

Hata hivyo, NCAA imejibu ikisema haijafanya usaliti wowote kwa wanafunzi waliopo kwenye orodha yao, fedha walishapeleka Halmashauri ya Ngorongoro yenye jukumu la kusimamia kulipa.

“Katika mkataba huo wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza wapo 400 hiyo ni kila mwaka kutoka shule 25 zilizopo vijiji 25 na kila kijiji kinatakiwa kutoa wanafunzi 16,” anasema Makamu Mwenyekiti wa NPC, Kitamwas Olemokotio.

Kitamwas anasema kila mwaka watoto wanaotakiwa kujiunga na kidato cha tano ni 33 ikiwa na maana kila kata watoto watatu kwa kata 11 za Tarafa ya Ngorongoro.

“Watoto wanaojiunga na vyuo vya kati ni 110 na wanaojiunga na vyuo vikuu ni 44 hiyo ni kila mwaka na wanaolipa ni NCAA na jukumu letu kama  Baraza tunatengeneza idadi ya wahitaji tunawapelekea,” anasema.

Anasema kwa mwaka 2024 walitekeleza matakwa ya mkataba huo lakini kinachowashangaza hadi sasa wanafunzi hawajapewa mahitaji yao na hata wale wa kidato cha kwanza licha ya elimu bure hawajapewa fedha ya matumizi.

 “Tukaja tukawapitisha wanafunzi 110 wa vyuo vya kati na watoto 33 wa kidato cha tano lakini hadi sasa hawajapewa fedha yeyote na wala kulipiwa ada tunashangaa changamoto hiyo inaanza kujitokeza mwaka huu wakati miaka mingine walikuwa wanalipia kama kawaida,” anasema.

Wakati akieleza hayo jana Jumatatu, Mei 20, 2024 wanafunzi sita wa vyuo vya kati na vikuu wanaosoma jijini Dar es Salaam ambao ni wenyeji wa tarafa ya Ngorongoro walitoka hadharani mbele ya vyombo vya habari jijini Dar es Salaam kueleza kilio chao cha kutolipiwa ada na fedha za kujikimu.

 “Kumekua na changamoto kubwa ya ulipaji wa ada na pesa za matumizi kwa wanafunzi wanaosomeshwa na baraza la wafugaji chini ya mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro.

“Mwaka jana baraza la wafugaji kupitia  kamati yake tendaji ilipitisha wanafunzi 154 na kati yao wanafunzi 55 pekee ndio wanalipiwa ada hasa wa vyuo vya kati wengine wote waliobaki 99 vyuo vya kati hali yao ni mbaya,”anasema Ezekiel Mamasita anayesoma mwaka wa kwanza Chuo kikuu cha Dar es Salaam.

Mwanafunzi mwingine kutoka chuo cha Tumaini, Tate Meiya anasema wanafunzi 55 vyuo vya kati na 44 vyuo vikuu hawajalipiwa ada wala kupewa fedha za kujikimu licha ya kupewa barua na mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro ya kupokelewa  vyuoni na kutambuliwa kama wafadhiliwa wa mamlaka hiyo.

“Hoja yetu hapa ni kwamba kwa nini NCAA waliowapa barua hawa wanafunzi  kupokelewa vyuoni kama bajeti yao ilikua hairuhusu? Kwa nini hawakusema mapema, watu wangejua namna nyingine ya kufanya” anasema.

Mwanafunzi mwingine kutoka chuo cha Dar es Salaam, Daniel Olopiro anasema kwa sasa wanapitia maisha magumu wakiwa chuo kwa kuwa walio wengi wanatoka familia zenye kipato cha chini.

“Tumesalitiwa tumetolewa Ngorongoro na kuja kutelekezwa huku ni bora wangetuambia mapema tungefanya kazi zingine badala ya kutuacha huku bila mahitaji yeyote, naingia semista ya pili hakuna siku nimewahi kulipiwa ada,”anasema

Kaimu Meneja uhusiano wa umma wa NCCA, Hamis Dambaya anakanusha madai ya kukiuka mkataba huku akieleza miaka yote wanalipia karo wanafunzi kutegemeana na ukubwa wa bajeti wanayopewa na Serikali.

Dambaya katika maelezo yake aliyoyatoa wakati akizungumza na Mwananchi Digital ametolea mfano mwaka wa fedha 2023/24, walitenga kiasi cha Sh1.3 bilioni kwa ajili ya kusaidia watoto 185 na katika idadi hiyo wanafunzi wapya kidato cha kwanza hadi cha tano 130.

“Wanafunzi wapya vyuo vya kati 55 tu, lakini kilichotokea idadi ya wanafunzi wapya walileta kama ilivyotakiwa lakini vyuo vya kati walileta idadi ya 154 wakati bajeti yetu ilikuwa 55 tu,” anasema.

Katika maelezo yake walisitisha kusaidia wanafunzi wa elimu ya juu kwa sababu Serikali inatoa mikopo, hivyo waliona ni muhimu nao waingie kwenye ushindani huo waombe ili kuipa nguvu mamlaka hiyo kusaidia wanafunzi wengi zaidi wa ngazi za chini.

Anasema baada ya kuletewa idadi kamili na Baraza hilo fedha wanapeleka moja kwa moja Halmashauri ya Ngorongoro wanaosimamia shughuli za kulipa karo na fedha za kujikimu.

“Tunachokifanya tukitenga bajeti yetu huwa tunawaandikia barua Baraza watupatie idadi kulingana na kiasi tulichotenga basi na fedha tunawasilisha Halmashauri wenye jukumu la kusimamia kwa wanafunzi waliokuwa kwenye idadi husika kuona wanalipiwa.

“Sasa kama hawalipwi kulingana na idadi tuliyowapa, hatujui lakini fedha tunatoa na wanaopaswa kuulizwa hapa ni Halmashauri ya Ngorongoro,”anasema

Akijibu hoja ya kuchelewesha kulipa karo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ngorongoro, Murtalah Mbillu amekiri kuwapo kwa changamoto hiyo inayosababishwa na mtandao, huku akijitetea yeye ni mgeni kwani ana miezi miwili tangu aanze kufanya kazi katika eneo hilo.

“Ni kweli kuna ucheleweshaji kwa wanafunzi lakini si kwa makusudi kwa mfano kwa sasa changamoto tuliyonayo ni mifumo malipo yaliingizwa tukayachakata haraka kwa sababu wako tofautitofauti kwa kusambaza na kuwapa malipo yao,” anasema.

Mbilu anasema kinachochelewesha malipo yao ni mifumo mathalani zilitangulia fedha zao za kujikimu lakini fedha za ada zinaleta changamoto kwa kuwa azma ya Serikali kila jambo lionekane katika utaratibu huo.

“Tunajitahidi kuongea na watu wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), wakiona yale malipo wayachakate yaweze kutoka haraka,”anasema.

Anasema fedha waliyoingiziwa ni Sh390.4 milioni na katika kiasi hicho kuna wanafunzi ambao hawastahili kulipiwa ada.

Akifafanua kuhusu fedha hizo, Mratibu wa Halmashauri ya Ngorongoro, Nade Thomas anasema Aprili mwishoni walipokea Sh390.4 milioni kiasi hicho kilikuwa kwa ajili ya wanafunzi wanaoendelea.

“Katika kiasi hicho Sh390.4 milioni kina upungufu wa Sh87 milioni ili kukamilisha idadi inayohitajika kwa wanafunzi wa vyuo vya kati 237 na vyuo vikuu 86,”anasema.

Anasema ili kutosheleza wanafunzi wote bajeti yao inatakiwa iwe Sh475 milioni na hawajapotokea yote kuasi cha kuweza kutosheleza wanafunzi.

“Kwa kujibu wa makubaliano yale Halmashauri kazi yetu tunahusika kulipa tu kile tunacholetewa na si kujua idadi halisi ya bajeti na anayepaswa kujua idadi ni mfadhili,”anasema.

Related Posts