Geita. Jeshi la Polisi Mkoani Geita limewakamata watu 567 wakituhumiwa kwa makosa mbalimbali yakiwemo ya mauaji, ubakaji, kukutwa na mali za wizi pamoja na dawa za kulevya aina ya bangi.
Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Saphia Jongo amesema watu hao wamekamatwa kwenye operesheni inayoendelea. “Operesheni hii ilianza Aprili mwaka huu, ni mwendelezo.”
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 21,2024 Kamanda Jongo amesema mbali na kukamatwa kwa watu hao pia wamekamata bangi kete 43 na gramu 520 pamoja na pombe ya moshi (gongo) lita 416.
Mali nyingine ni mashine ya kusagia mawe, pikipiki nane vitenge majora 15, televisheni nane, magodoro matano, kompyuta nne, mafuta ya dizel lita 65 na cherehani mbili.
Akizungumzia udhibiti wa ajali barabarani Kamanda Jongo amesema kwa kipindi cha Aprili makosa 8,124 ya usalama barabarani yametokea.
Amesema pamoja na kuwakamata watuhumiwa bado kwenye kesi za ubakaji kuna changamoto ya mashahidi kwenda kutoa ushahidi, kutokana na baadhi kupenda kumalizana nyumbani
“Tumepandisha kesi mahakamani zipo zinazoendelea na zilizotolewa hukumu ila zilizopo sasa ni za mauaji, bangi na kubaka ambazo zinahitaji uchunguzi wa madaktari na mashahidi, ila wanaopaswa kutoa ushahidi wanapenda kuelewana nyumbani ndio tunasumbuana nao kufika mahakamani kutoa ushahidi,”amesema.
Kamanda Jongo amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi na kuliamini ili kutokomeza uhalifu kwenye mkoa huo.
Wakizungumza hali ya usalama mkoani humo baadhi ya wananchi wameiambia Mwananchi Digital kuwa jeshi hilo limejitahidi kupambana na uhalifu wa nyumba kwa nyumba uliokuwa ukifanywa nyakati za usiku, na sasa watu wanalala kwa mani.
Manjale Kazamoyo mkazi wa Mtaa wa Mission Mjini Geita amesema ipo haja ya Serikali kutunga sheria za kuwabana watu wanaomalizana na wahalifu nyumbani hususan kwenye kesi za ubakaji, kwa kuwa wao ndio wanaochangia matukio haya kuendelea.
“Huku usukumani hili la kumalizana na mhalifu familia wanapewa fedha au ng’ombe limezoeleka sana na asilimia kubwa wazazi ndio wanapewa, lakini aliyefanyiwa ukatili wa kubakwa anakuwa hana cha kufanya anaweza kuozeshwa kwa nguvu au akabaki tu nyumbani.”
“Serikali iliangalie jambo hili kwa undani ili haki iweze kutendeka,”amesema Kazamoyo.