Watumishi 25,039, taasisi 65 wahamia Dodoma

Serikali imesema hadi sasa, jumla ya watumishi 25,039 kutoka Serikali kuu, Bunge, mahakama, vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na taasisi 65 wameshahamia Dodoma na wanaendelea kutekeleza majukumu yao wakiwa makao makuu ya nchi. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Hatua hiyo imekuja baada ya zoezi la kuhamisha makao makuu ya Serikali kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma lilianza rasmi mnamo mwaka 2016.

Mbunge wa Bahi, Kenneth Nollo (CCM).

Hayo yamebainishwa leo Jumanne na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Ummy Nderiananga wakati akijibu swali la Mbunge wa Bahi, Kenneth Nollo (CCM), aliyehoji ni lini zoezi la kuhamia Dodoma litakamilika na ni taasisi ngapi zimeshahamia Dodoma.

Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri huyo amesema Serikali inatarajia kukamilisha mpango wake wa kuhamia makao makuu ya nchi Dodoma kwa kuzingatia Mpangokazi maalum na ujenzi wa awamu ya pili wa majengo ya Ofisi za Wizara na Taasisi utakaohitimishwa ifikapo mwaka 2025.

Akizungumzia kuhusu ujenzi wa nyumba za viongozi na watumishi, amesema mwaka 2021/2022 Serikali ilijenga nyumba 20, mwaka  2023 ilijenga nyumba 150 na mwaka huu tayari imetenga hekari 4,656 katika eneo la Mtumba ili kuendeleza mji huo wa Serikali.

Related Posts