Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeanza kusaka mwarobaini kudhibiti matumizi ya simu za mkononi wakati wa muda wa kazi na kuhakikisha kunakuwa na matumizi mazuri ya mitandao.
Hayo yamebainishwa leo Jumanne Mei 21, 2025 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman wakati wa mkutano wa 15 wa Baraza la Wawakilishi unaoendelea Chukwani, Zanzibar.
Hatua hiyo imekuja baada ya mchango wa Mwakilishi wa Kwerekwe, Ameir Abdalla Ameir ambapo amesema miongoni mwa changamoto kubwa ya utumishi wa umma Zanzibar ni pamoja na kutotumia ipasavyo muda wa kazi.
“Watumishi hujishughulisha na mambo yasiyohusiana na masuala ya kazi, bila ya kujali kuwa wanafanya makosa na uzembe kazini,” amesema.
Ametaka kujua kwa kiasi gani uzembe wa kutotumia muda ipasavyo kwa watendaji wa Serikali unakwaza na kuzorotesha maendeleo ya jamii na taifa.
“Ni kweli kwamba, uzembe wa kutotumia muda ipasavyo kwa watendaji wa Serikali unakwaza na kuzorotesha maendeleo ya jamii yetu kwa kiasi kikubwa na kutokana na tatizo hilo hupelekea matokeo mengi mabaya yakiwemo kutokuwa na ufanisi wa utendaji kazi, jamii kukosa huduma kwa wakati na kutofikia malengo ya taasisi na Serikali kwa jumla,” amesema Suleiman.
Amesema Serikali inaendelea kuchukua jitihada mbalimbali ikiwa ni pamoja kutafuta njia bora za kudhibiti matumizi ya simu za mkononi muda wa kazi na pia kuhakikisha kunakuwa na matumizi mazuri ya mitandao.
Amesema, wiki chache zilizopita Serikali imetoa toleo maalumu juu ya suala hilo.
“Hivi sasa, tumeshaanza kuzifanyia kazi hoja zilizoibuka na kuzingatia maoni pamoja na mapendekezo mbalimbali tunayoendelea kupokea na kusikia juu ya hatua hii tuliyoichukua,” amesema.