Unguja. Ili kukabiliana na uhaba wa vitabu vya kusomea na kujifunzia katika shule za msingi na sekondari, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar (Wema), imetenga Sh200 milioni kutengeneza mifumo maalumu ya maktaba mtandao.
Mifumo hiyo ijulikanayo E-Library system & Library Management System, itawezesha wanafunzi kupata maudhui mbalimbali kwa njia ya mtandao.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ali Abdulgulam Hussein ametoa kauli hiyo leo Jumanne, Mei 21, 2024 katika Mkutano wa 15 wa bajeti mwaka 2024/25 wa Baraza la Wawakilishi Chukwani mjini hapa.
Amesema kiasi hicho cha fedha kitasaidia kutengeneza mifumo hiyo ya kielektroniki ambayo itarahisisha utoaji wa huduma za maktaba kuanzia shule hadi maktaba za jamii.
Amesema kwa kuanzia maktaba mtandao, zitaanza na shule 30 ambapo katika kila shule zitawekwa kompyuta mpakato 26, tv za kisasa na vifaa vyote muhimu vya kielektroniki.
“Hii ni kupitia mradi wa mageuzi ya Elimu Kidijitali (DEP-MZES) unaotekelezwa kwa ushirikiano na Austria, na utekelezaji mradi huu umeanza Machi 2024,” amesema Naibu Waziri Ali
Ali ametoa maelezo hayo wakati akijibu swali la mwakilishi wa Kwerekwe, Ameir Abdalla Ameir aliyetaka kujua mpango wa Serikali kuwapatia wanafunzi maktaba mtandao ili kuondokana na tatizo la uhaba wa vitabu vya kusomea na kujifunzia.
Hata hivyo, Mwakilishi huyo ametaka kujua vigezo vilivyotumika kuzipata shule hizo huku Zanzibar kukiwa na changamoto kubwa ya intaneti wakati mfumo huo unahitaji mtandao imara uweze kufanya kazi.
Kadhalika Mwakilishi wa Mwera, Mihayo Juma Nhunga amepata wasiwasi kuhusu mpango huo akisema bado kuna vituo maalumu vya amali ambavyo wanatumia intaneti za vifurushi binafsi na kuongeza gharama kwa watumiaji.
Naibu Waziri alisema kuna miradi mwili inayofanyika ambayo itasaidia kuongeza intaneti na kwa sasa wanafanya upembuzi yakinifu kuangalia shule ambazo zitapewa kipaumbele, kulingana na mazingira ya upatikanaji wa intaneti kwa urahisi.