MUDA mchache baada ya uongozi wa Mashujaa FC kuweka bayana kuachana na kinara wa mabao wa timu hiyo, Adam Adam mchezaji huyo amevunja ukimya na kufunguka kilichomng’oa.
Mshambuliaji huyo mwenye mabao saba katika Ligi Kuu ambaye mkataba alionao na klabu hiyo unaisha mwisho wa msimu huu, ameliambia Mwanaspoti ameachana na timu hiyo baada ya kuomba ruhusa ya kupumzika kuuguza jeraha la nyonga.
“Ni kweli nimeachana na Mashujaa, baada ya kuomba mapumziko kutokana na kusumbuliwa na nyonga na uongozi umenikubalia,” amesema Adam na kuongeza;
“Nimekuwa nikisumbuliwa na tatizo hili kwa muda sasa na ukiangalia Ligi inaenda mwisho, sioni nikicheza mechi zilizobaki, hivyo nikaamua kuomba ruhusa ambayo ni hadi mwisho wa msimu hivyo wakaona wamalizane nami kabisa.”
Nyota huyo wa zamani Tanzania Prisons na KMC amezungumzia maisha ndani ya klabu hiyo, kwamba yalikuwa ya ushirikiano, hivyo anawatakia wachezaji wenzake kumaliza ligi kwa amani na waendeleze mapambano kwa kuhakikisha timu hiyo haishuki daraja.
“Naamini wachezaji wenzangu watafanya kazi nzuri ya kuipambania timu, ili ifikie malengo yake,” amesema.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari na Mawasiliano ya klabu hiyo imethibitisha kuachana na mshambuliaji huyo kwa makubaliano maalum ya pande zote mbili na kumtakia kila la kheri kwenye safari yake ya mchezo wa soka.