Dk Bagonza: Hata viongozi wa dini wanahitaji msaada

Dar es Salaam. Wakati kukiwa na mjadala kuhusu matukio ya hivi karibuni ya watumishi wa Mungu kujiua, viongozi wa dini wameeleza wao pia ni binadamu wenye changamoto zinazowakabili, hivyo isionekane ajabu wanapohitaji msaada.

Viongozi hao wameweka bayana kama ilivyo kwa binadamu wengine hata wao kuna wakati hupata msongo wa mawazo, hivyo ni muhimu kukawa na mfumo madhubuti wa kuwasaidia.

Wamesema isiwe jambo la kushangaza wanapoweka                     wazi yanayowakabili.

Kumeibuka mijadala ndani ya jamii ikiwamo kwenye mitandao ya kijamii kutokana na matukio ya kujinyonga askofu na frateri.

Mei 20, 2024 frateri wa Shirika la Roho Mtakatifu la Kanisa Katoliki Jimbo la Tanga, Rogassion Massawe alidaiwa kujinyonga akiwa kwenye nyumba ya malezi na kuacha ujumbe kwa mama yake akieleza kushindwa kufikia malengo.

Tukio la awali ni la Mei 16, 2024 lililotokea jijini Dodoma ambako Askofu Mkuu wa Makanisa ya Methodist, Joseph Bundala (55) alidaiwa kujinyonga na kuacha ujumbe ulioleza sababu ya kuchukua hatua hiyo ni kuzidiwa na madeni na mgogoro wa shule binafsi aliyoiuza.

Kauli ya viongozi wa dini

Akizungumza na Mwananchi kuhusu mjadala huo, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Benson Bagonza amesema mjadala huo ni matokeo ya kuwa na jamii inayoamini viongozi wa dini hawana matatizo bali wanapaswa kutatua changamoto za wengine.

“Tunaishi katika jamii inayoamini viongozi wa dini hawana matatizo, wana majibu ya kila kitu, hii siyo kweli. Hata wao ni binadamu kuna wakati wanapitia magumu katika maisha, wanakimbilia wapi kupata suluhisho?” amesema Bagonza.

“Katika mfumo wa kiroho anaweza kutubu pale anapojiona amefanya dhambi lakini vipi kuhusu maisha ya kawaida na masuala ya kijamii, jibu ni kwamba hatuna mfumo kuwatunza wanaotunza wengine.”

wenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka.

Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka amesema kama ilivyo kwa binadamu wengine, viongozi wa dini nao wapewe fursa ya kujadili mambo yao kijamii ili wanapokwama waweze kusema.

“Maisha ya viongozi wa dini yameingiliwa na mfumo wa kimaisha ikiwamo utandawazi. Uwezo wa kiimani haujengwi ipasavyo, hivyo kiongozi wa aina hii anapopata tatizo anaona bora abaki nalo na ubinadamu unapomshinda ndiyo anachukua hatua mbaya,” amesema Sheikh Mataka.

“Kwa kawaida binadamu anapokumbana na mambo yanayoathiri akili yake anarudi kuwa mnyama. Hasira, kukata tamaa vyote hivi vinaathiri akili ya binadamu na kama hana wa kushauriana naye atajikuta akichukua uamuzi usiofaa,” amesema.

Daktari wa Afya ya Akili, Pascal Kang’iria amesema suala hilo lina uhusiano mkubwa na changamoto ya afya ya akili, hivyo kama ilivyo kwa makundi mengine elimu inapaswa kuwafikia pia viongozi wa dini.

“Tuondokane na zile fikra za kizamani kwamba viongozi wa dini hawana matatizo, elimu ya afya ya akili inapaswa kuwafikia watu wote ili kuepusha matatizo ya aina hii. Kuna kila sababu ya kujifunza namna za kukabiliana na misongo ya mawazo na kuwasaidia wale wanaoonekana na dalili za hatari,” amesema Dk Kang’iria.

Dalili za mtu anayetaka kujitoa uhai

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) zipo dalili kadhaa zinazoweza kuashiria mtu anataka kujitoa uhai.

Baadhi ya hizo ni kulala sana, kujitenga na wengine na mara nyingi hujifanyia mambo kivyake, hupoteza matumaini ya kuishi, hujiona hana msaada, thamani na kujichukulia kuwa mzigo kwa wengine au kuzungumzia kukosa umuhimu wa kuishi.

Mkurugenzi wa Asasi ya Tap Elderly Women’s Wisdom for Youth (TEWWY), Rustika Tembele amesema Tanzania inaweza kukabiliana na matukio ya watu kujiua endapo jamii itarudi kwenye msingi wa maisha ya upendo na ujamaa.

Amesema matukio hayo yanaendelea kutokea wakati yangeweza kuzuilika kwa kuwa mtu anayefikia kujiua hafikii uamuzi huo bila kuwepo sababu.

“Mfumo wa maisha umebadilika, watu hawajali shida za wengine ndiyo kwanza wanafurahia kumbe hujui yule unayemfurahia matatizo yake ungekuwa naye karibu kumfariji huenda asingefikia uamuzi wa kujiua,” amesema Tembele.

Amesema ni muhimu kwa wanajamii kuwapa matumaini watu walioelemewa na mizigo kwenye mioyo ili kuwanusuru na matatizo ya afya ya akili ambayo yanaweza kumsukuma mtu kujitoa uhai.

Askofu Bagonza ameshauri viongozi wa dini kuepuka kuzungukwa na watu ambao hawawezi kumwambia ukweli, badala yake wanaishia kumpa sifa zisizo za kweli.

“Ukiwa kiongozi unayezungukwa na watu ambao hawawezi kukwambia ukweli hilo ni tatizo, lazima wawepo ambao wana uthubutu wa kukwambia mambo usiyotaka kuyasikia. Wawepo watu wanaoweza kukwambia kwamba unakopa sana, unawasumbua waumini, madeni yanakuzidi uwezo,” amesema Askofu Bagonza.

Ameshauri taasisi za dini kuwa na utaratibu wa siri au wa wazi wa kuwasaidia viongozi wao ili wawe huru kuzungumza wanapokabiliwa na changamoto za kibinadamu.

Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Jackson Sosteness amesema kuwa kiongozi wa dini hakuondoi ubinadamu wa kiongozi husika katika kukabiliana na changamoto za kibinadamu.

“Kiongozi mwenyewe unapaswa kutambua wewe ni binadamu, pia uwe tayari kuomba msaada kwa wengine. Kama ni binadamu changamoto ni kawaida, ni kweli huwezi kuweka mambo yako wazi kwa kila mtu lakini jitahidi kuwa na mtu unayeweza kuzungumza naye akakushauri kwa yale unayoyapitia,” amesema.

Related Posts