NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,amewataka Wajumbe wa Sektetarieti za CCM ngazi za Matawi, Wadi na Jimbo la Kwahani kuendeleza utamaduni wa kufanya kazi za Chama na Jumuiya zake kwa ubunifu na uchapakazi katika majukumu yao ya kila siku.
Nasaha hizo amezitoa wakati akizungumza na wajumbe hao katika ziara yake ya kuimarisha uhai wa Chama Cha Mapinduzi katika Jimbo la Kwahani Unguja, alisema kila mtendaji na kiongozi wa CCM anatakiwa kutekeleza wajibu wake ili kuwa mfano bora na wa kuigwa kwa wanachama na makada wa Chama hicho.
Dkt.Dimwa, alieleza kuwa CCM itaendelea kusimamia wajibu wake wa kuwa daraja la kuwaunganisha wananchi na Serikali zake mbili ili jamii iwe na uelewa mzuri wa kufahamu utekelezaji mkubwa wa kazi za kimaendeleo unaofanywa na Serikali zilizopo madarakani.
Katika maelezo yake Dkt.Dimwa, alisema kasi kubwa ya maendeleo kupitia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 unaofanyika nchini hivi sasa imekuwa ni tishio kwa Vyama vya upinzani na kupelekea kuanza kutoka nje ya mstari kwa kutoa tuhuma sisizokuwa za kweli kwa baadhi ya viongozi wa Serikali na Chama kwa ujumla.
“ Kasi yetu ni ile ile yenye viwango vya siasa za kisayansi mpaka mwaka 2025 hatusimami hadi tutakapohakikisha tunashinda uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Hivyo wito wangu kwenu tekelezeni majukumu yenu ipasavyo kwa mujibu wa miongozo na Katiba yetu ya mwaka 1977 toleo la Disemba 2022, msivunjwe moyo wala kuteteleka kwa mbwembwe na kelele za Wapinzani wanaona CCM imeshajibu hoja zao kwa vitendo na wanaanza kutafuta huruma ya kisiasa kwa kususia uchaguzi mara kudai Katiba mpya sisi tunasonga mbele.”, alieleza Dkt.Dimwa.
Pamoja na hayo alitoa wito kwa wanachama,viongozi na makada wa CCM wa Jimbo la Kwahani kujiandaa Kisaikolojia juu ya kuyafanyia kazi kwa vitendo maelekezo ya Chama na Jumuiya zake wakati yatakaposhushwa kwa ajili ya utekelezaji.
Aidha, aliwasihi wananchi bila kujali tofauti za kisiasa, kidini na kikabila kuendeleza utamaduni wa kulinda amani na utulivu wa nchi ili kupata fursa pana ya kutekeleza majukumu yao ya kujipatia kipato halali kwa wakati.
Kupitia ziara hiyo, aliwapongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Mwinyi, kwa utendaji wao mzuri ulioongeza ufanisi katika uimarishaji wa nyanja za kiuchumi, kijamii, kisiasa na kidiplomasia kwa ujumla.
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,akisisitiza juu ya kufuata ya Katiba ya CCM mwaka 1977 toleo la Disemba 2022 wakati akizungumza na Wajumbe wa Sekretarieti za CCM ngazi za Matawi, Wadi na Jimbo la Kwahani Unguja katika ziara yake ya kuimarisha uhai wa Chama Cha Mapinduzi iliyofanyika Tawi la CCM Muungano Wilaya ya Mjini Zanzibar