Fyatu Mfyatuzi, mwanazuoni, mzalendo, na mwanamapinduzi asiye kifani, nimejitoa kuchangia madini ya kuondokana na mgongano-muungano. Sihitaji kukaribishwa wala kulipwa kusaidia kufanikisha azma ya kuwa na kaya tulivu yenye mshikamano ambavyo haviwezi kupatikana kwa kuogopana, kudanganyana, kuzidiana akili au kufyatuana ilivyo.
Muungano unataka vichwa vinavyochemka, ukweli, ushupavu, uwazi, uzalendo na utayari kufanya ambacho kimombo huitwa ‘give and take to reach a win-win conclusion’. Walipounganika Juliachi Nchonga aliogopa ‘eti’ kuimeza Zenj akaiacha kinamna iimeze Tanganyika. Tusipokuwa wakweli na wawazi, tutauvunja huu mgongano. Hili halina ubishi.
Siyo dharau au kusahau mchango na wema wa Mzee Nchonga na Abby Karumekenge kayani. Nijuavyo, Nchonga hana historia ya muungano. Waliobukua historia ya Afrika wanamkumbuka kama shujaa mwoga aliyekwamisha muungano wa Afrika akihofia kupoteza madaraka, tofauti na Kwami Nkrumah aliyetaka kuunganisha Afrika mara moja.
Katika mkutano na mtifuano baina ya wawili hawa, kulikuwa na kujipiga vifua, kupingana, kukwaruzana, hata kukwazana na kuhujumiana. Bila elements kama Nchonga, Afrika ingekuwa moja. Aliturithisha woga na kiini macho. Sasa tuna bonge la sheshe.
Tatizo, wakati ule na sasa ni kwamba Afrika ilirithi viinchi uchwara walivyotengeneza wakoloni kule Berlin Ujerumani kwa faida na sababu zao.
Nkrumah alitaka, kama ambavyo Afrika ilikatwa vipande kwa wakati mmoja, vivyo hivyo, ilipaswa kuuganishwa upya na kurejea muungano wake wa asili. Tofauti, Mzee Nchonga alitaka muungano mdomdo ambao matokeo yake ni kushindwa kuunganisha Afrika na kung’ang’ania mataifa, utambuliko na muundo wa kikoloni.
Mwanazuoni nguli, Issa Shivji kwenye andiko; Pan-Africanism or Imperialism? Unity and Struggle towards a New Democratic Africa (2006) anasema: “Nkrumah believed, not unreasonably, that regional groupings and associations would make continental unity even more difficult while Nyerere seemed to subscribe to the gradualist approach holding that any form of unity among any number of African states was a step in the direction of African unity.”
Tafsiri: “Nkrumah aliamini, siyo kijinga, kuwa makundi na mashirikiano ya kijimbo yangefanya uunganishaji wa bara kuwa mgumu zaidi wakati Nyerere aliamini katika uunganishaji mdomdo, akishikilia kuwamba aina yoyote ya muungano wa idadi yoyote ya mataifa ya Kiafrika ilikuwa ni hatua kuelekea muungano wa Afrika.”
Sababu za magwiji hawa ilikuwa ni siasa za wakati ule realpolitik na geopolitics. Kama tumejifunza tokana na madhaifu yao tukashindwa kufanya tofauti, nasi hatuna tofauti na wakoloni au mawakala wao kwa kung’ang’ania utaifa uliotengenezwa na mkoloni katili, mnyonyaji na katili.
Tunapaswa kujivua ukoloni na kuuona ukweli na uhalisia ili tusonge mbele.
Changamoto, mazingira, mahitaji na hatima vya muungano na sababu zake za sasa ni tofauti na zile zilisababisha kuundwa kwake kitaifa na kimataifa. Mfano, hakuna tena kambi hasimu hasimu za Magharibi na Mashariki wala kitisho cha Zenj kuchukuliwa na kambi ya Mashariki au wamanga waliotemeshwa ulaji na kuwa tishio kwa maslahi ya Danganyika au ya kambi ya Magharibi kama ilivyokuwa wakati ule.
Pili, Wadanganyika na Wazenj sasa wana uelewa mkubwa wa mambo kuliko wa wakati ule.
Hata hawa wanaotaka kuusaidia muungano wakaonekana maadui wa kulaaniwa hata kutengwa, wana uwezo na uwanja mpana wa kujieleza bila woga wala unafiki.
Tatu, mahitaji ya sasa ya taifa na muungano ni tofauti na ya wakati ule. Sasa tuna kizazi kilichoelimika, kufyatuka na kisichoogopa wala kuficha kitu.
Nne, uzoefu wa muungano nao pia una mchango mkubwa katika kuamua hatima yake. Mfano, tangu uundwe, umekuwa mgongano zaidi ya muungano.
Umejenga ubaguzi baina ya pande mbili hata kama ni kwa bahati mbaya au makusudi.
Umetumika kisiasa na si kwa kila nyanja, yaani kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Umebinafsishwa kwa chama kimoja, wakati huu ni wakati wa demokrasia ya vyama vingi. Wanaoupinga wana haki sawa na wanaounga mkono. Kinachogomba ni kwa nini wanafanya hivyo. Hivyo, suluhisho mojawapo na kuwa na muungano bora tunaoutaka kwa faida sawa kwa wote ni kukubali kukosoana, kutofautiana na kuambizana ukweli na tukausikiliza na kujibu hoja kwa hoja badala ya ujinga na kutishana.
Tano, changamoto na kero za muungano hazitaondoka zenyewe. Haziepukiki. Kwenye taaluma ya utatuzi wa migogoro tunasema kuwa hali na mchakato kama hivi ni katili, ngumu na chafu (brutal, complex, messy).
Lazima tukubali haya ili tuweze kufanya kitu cha maana, kufaidika na kusonga mbele.
Nimalizie, katika muungano wa kweli hakuna Wadanganyika wala Wazenj bali Watanzania. Sheria ya 1984 Na.15 (ib. 1) inasema, ninukuu: “Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano” (uk. 11) iliyoua na kumeza Tanganyika na Zanzibar na kuzaa utanzania. Lipi gumu hapa yarabi?! Kama sisi ni kaya moja, sirkal mbili za nani na nini? Du! Hivi niko wapi?