IDADI YA WANAOSAJILI MAJINA, NEMBO NA BUNIFU ZAO YAONGEZEKA

Na Gideon Gregory , Dodoma.

Ofisa Habari Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Theresia Chilambo amesema kwasasa muitikio wa watu kusajili bidhaa zao umeongezeka tofauti na kipindi cha nyuma kwani imefikia hatua ambayo watu wanasajili majina yao pamoja na alama wanazozibuni ili kuepuka wizi wa bunifu za watu ambao umekuwa ukijitokeza.

Bi. Theresia ameyasema hayo Jijini Dodoma kwenye maonesho ya wiki ya Viwanda na Biashara katika Viwanja vya Bunge Jijini Dodoma.

Amesema lengo la kushiriki kwenye maonyesho hayo ni kutoa elimu kwa wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi kuhusu masuala ya urasimishaji biashara.

“Lengo letu sisi kama BRELA kushiriki katika maonesho haya ni kuweza kuwaelezea wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi kwani tunajua tukishawapa elimu hawa wabunge masuala ya uelimishaji au urasimishaji biashara katika sekta ya biashara, viwanda na uwekezaji basi watakuwa mabalozi wazuri”,amesema.

Pia amesema kupitia maonesho hayo yatasaidia kutoa huduma kwa wabunge ambao wanamiliki biashara kuzisajili pamoja na kuhuisha taarifa mbalimbali kwa msajili wa makampuni.

Aidha ameongeza kuwa kupitia usajili wa kidigitali waliouanzisha umewesha usajili kuwa rahisi sehemu yoyote anapokuwa na lengo la kufanya hivi ni kuendana na ukuaji wa teknolojia unaoendelea na kuongeza kuwa mfumo huo unatumia lugha zote ikiwemo Kiswahili na Kingeleza.

Related Posts