Jaji Mkuu, DPP watoa miongozo kesi za Plea Bargaining

SERIKALI imetunga kanuni na miongozo mipya kuhusu uendeshaji mashauri yanayomalizika kwa mshtakiwa kukiri kosa (Plea Bargaining), ili kumaliza changamoto zake zilizoibuliwa na wadau tangu utaratibu huo uanze kufanya kazi 2019. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Hayo yamebainishwa leo tarehe 22 Mei 2024, bungeni jijini Dodoma na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Eliezer Feleshi, baada ya Mbunge wa Mbagala, Abdallah Chaurembo (CCM), kuishauri Serikali ifanye tathmini ili kubaini changamoto zinazotokana na utekelezaji wa Plea Bargaining.

Dk. Feleshi amesema Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Sylvester Mwakitalu, wameandaa miongozo na kanuni ya kushughulikia kesi hizo.

“Ni vizuri mbunge akaelewa changamoto za awali zimeshatatuliwa baada ya jaji mkuu kutoa kanuni za kushughulikia mashauri yanayoishia kwa njia ya kukiri, pamoja na DPP kutoa miongozo ya kuongoza waendesha mashtaka na wapelelezi namba ya kushughulikia. Mengine yanayoendelea kuibuka yataendelea kuanguka kwenye mkondo unaoendelea wa kufanyiwa kazi na Serikali,” amesema Dk. Feleshi.

Aidha, Dk. Feleshi amesema changamoto za Plea Bargaining ni miongoni mwa masuala yaliyojumuishwa katika ripoti ya tume ya haki jinai iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassa, ili zikafanyiwe kazi kwa ajili ya maboresho.

Mbunge wa Mbagala, Abdallah Chaurembo (CCM).

Awali, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini, alisema Plea Bargaining ilianza kutekelezwa 2019  baada ya Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai kufanyiwa mabadiliko kwa kuongezwa vifungu vya 194 (A,B,C) vilivyoanzisha utaratibu wa kukiri makosa kwa makubaliano maalum kati ya mshtakiwa na Serikali.

Sagini amesema lengo la Plea Bargaining lilikuwa ni kupunguza muda wa upelelezi na usikilizwaji wa mashauri, kupunguza mlundikano wa mahabusu, kuwezesha kubaini namna uhalifu unavyotendeka na kubaini mtandao wa uhalifu.

Naibu waziri huyo wa katiba na sheria amesema, tangu utaratibu huo wa kukiri kosa uanze kufanya kazi (2019 hadi Juni 2023), mashauri 423 yaliyohusisha watuhumiwa 1,040 yalimalizika na kuwezesha fedha kiasi cha Sh. 54.64 bilioni kurejeshwa serikalini.

Related Posts