Dodoma. Mbunge wa viti maalumu (CCM), Esther Malleko ameihoji Serikali ni lini itafanya maboresho ya Sheria ya Ndoa ili ikidhi matunzo kwa watoto kwa sababu gharama za maisha zimepanda.
Akiuliza swali leo Jumatano, Mei 22, 2024, Malleko amehoji: “Nini kauli ya Serikali kwa wale wanaoshindwa kutekeleza majukumu waliyokubaliana katika vikao vya usuluhishi na kusababisha watoto kupata shida.”
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini amesema sheria ni ya mwaka 1971 hivyo viwango vilivyowekwa kwa wakati huo vinaweza vikawa vimepitwa na wakati.
“Tulichukue na tuielekeze Tume ya Marekebisho ya Sheria katika maboresho ya Sheria ya Ndoa wanayoyafanya hivi sasa, wazingatie na viwango hivi ili viende kwa wakati,”amesema Sagini.
Kuhusu kutotekelezwa kwa makubaliano, Sagini amesema anayeona makubaliano hayatekelezwi anapaswa kwenda mahakamani kwa sababu ndiyo inayopaswa kutenga viwango kwa ajili ya matunzo ya watoto.
Katika swali la msingi, Malleko amehoji ni upi mkakati wa Serikali wa kuimarisha huduma za usuluhishi kwa migogoro ya ndoa na matumizi ya watoto.
Akijibu swali hilo, Sagini amesema kwa mujibu wa kifungu cha 102 cha Sheria ya Ndoa Sura ya 29, waziri mwenye dhamana na masuala ya Sheria amepewa mamlaka ya kuanzisha Mabaraza ya Usuluhishi wa Ndoa katika kila kata au sehemu nyingine atakayoona inafaa.
Aidha, amesema mabaraza hayo yameanzishwa na yanafanya kazi katika kata zote nchini.
Amesema pia kifungu cha 101 cha Sheria ya Ndoa Sura ya 29, mgogoro wowote wa ndoa lazima upitie katika hatua ya usuluhishi kabla ya kuwasilishwa mahakamani.
Amesema mabaraza hayo yana mamlaka ya kusuluhisha migogoro ya ndoa ikiwamo matunzo ya watoto.